Na Mwandishi Wetu
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza matokeo ya Tume Huru ya Uchunguzi iliyoundwa kuchunguza matukio ya Oktoba 29, mwaka, yataongoza hatua ya serikali katika uwajibikaji, maridhiano na mageuzi ya taasisi.
Pia, alisema serikali itaendelea kusimamia mchakato wa maridhiano, yakiwemo majadiliano kupitia majukwaa yaliyopo kisheria na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.
Rais Dk. Samia alitoa msimamo huo juzi jioni, alipopokea ujumbe maalumu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalumu, Rais Mstaafu wa Malawi, Dk. Lazarus Chakwera, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ujumbe huo umeainisha maeneo ya kipaumbele yanayofuatiliwa na Jumuiya ya Madola, ikijumuisha uwazi na ushirikiano katika tathmini ya matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana na kupanua ushiriki wa kisiasa, kuendeleza majadiliano ya vyama na kuimarisha uwajibikaji wa taasisi.
Katika ujumbe wake, Shirley alisisitiza dhamira ya Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na maridhiano ya kitaifa kufuatia matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana.
Alisema Jumuiya ya Madola inaunga mkono juhudi zinazoendelea nchini na iko tayari kusaidia kujenga mazingira ya kisiasa yenye utulivu, ushirikishwaji na kuaminiana kupitia mazungumzo na mageuzi ya taasisi.
RAIS DK. SAMIA
Akizungumza wakati wa kupokea ujumbe huo, Rais Dk. Samia alisema Tanzania inaendelea kushughulikia hali hiyo kupitia taasisi zake, huku akitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali, ikiwemo kuunda Tume Huru ya Uchunguzi kurejesha utulivu na kuimarisha uwajibikaji nchini.
Alisema serikali itaendelea kusimamia mchakato wa maridhiano, yakiwemo majadiliano kupitia majukwaa yaliyopo kisheria na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Chakwera alieleza utayari wa Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na Tanzania katika juhudi za kuimarisha utawala wa sheria, ushirikiano wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa.
Katika hatua nyingine, Chakwera, amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tisa nchini, kama Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, kufanya tathmini ya hali ya kisiasa na mchakato wa maridhiano, ambapo alikutana na wadau mbalimbali wa siasa na taasisi za kiraia nchini




