Na NASRA KITANA
KLABU ya Yanga juzi imekabidhiwa sh. Milioni 60 za ‘Goli La Mama’, ikiwa ni zawadi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itokanayo na ushiriki wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Katika mashindano hayo, Yanga waliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mchezo wa mwisho walishinda mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie ya nchini Algeria uliochezwa katika Uwanja New Amaan, Complex visiwani Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi fedha hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema kuwa amekabidhi fedha hizo kutokana na magoli ambayo Yanga walifunga magoli katika mashindano hayo.
Katibu huyo alisema kuwa anawatakia kila la kheri Yanga katika mechi zake za Ligi Kuu msimu huu kufanya vizuri na kupambania nafasi yao ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Leo katika mechi dhidi ya Mbeya City tumekabidhi millioni 60 ikiwa ni zawadi ya Rais Dk. Samia kwa magoli yote waliyoyapata katika mashindano ya kimataifa msimu uliopita na kuishia hatua ya makundi,” alisema Msigwa.
Naye Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Saidi alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk. Samia kwa fedha hizo kwani itawaongezea motisha kueleka katika michuano hiyo msimu ujao.
“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa zawadi yake ya Goli la Mama, tunatambua mchango wake katika maendeleo ya soka, katika kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika kuendeleza soka la Tanzania, tunatarajia kushiriki mashindano ya vijana kupitia mradi wa Yanga Soccer School. Tunamhakikisha Rais Samia kuwa tupo mstari wa mbele katika kukuza na kuinua soka la Tanzania, “ alisema Hersi.
Yanga ambayo iliishia hatua ya makundi ilianza mechi zake za hatua hiyo kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya FAR Rabat, ikakubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly, ikapata suluhu dhidi ya Js Kabylie, ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly, ikafungwa bao 1-0 na timu ya FAR Rabat na kushinda mabao 3-0 dhidi ya Js Kabylie.
BAADA YA KUIFUNGA MBEYA CITY
Baada ya kupata ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mbeya City, kocha wa Yanga Pedro Goncalves, amesema presha yake imeshuka na ana furaha kuona wachezaji wake wanajituma na kutumia vizuri nafasi ambazo wamezipata.
Yanga juzi ilishinda mabao 6-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumalizika mchezo huo, Pedro alisema kabla ya kikosi chake kuingia uwanjani aliongea na wachezaji wake huku akiwataka kuhakikisha wanapambana kufikia kiwango waliojiwekea.
Kocha huyo alisema alihitaji kuona timu yake inafanya vizuri katika kila mchezo kuhakikisha wanatetea taji la ubingwa la ligi hiyo.
“Haikuwa kazi rahisi kwetu kupata ushindi wa mabao mengi, lakini niwapongeze wachezaji wangu kwa kuendelea kufuata maelekezo ambayo ninawapatia,” alisema Pedro.
Kocha huyo alisema katika kikosi chake, anataka kuona kila mchezaji anapambana na kutumia vyema nafasi ambayo anaipata kuonesha uwezo wake.
MBEYA CITY WAMTIMUA KOCHA WAKE
Wakati huo huo, uongozi wa Mbeya City umemfungashia virago kocha wake, Mecky Maxime pamoja na wasaidizi wake ambao ni Nizar Khalfan na Francis Mkanula.
Uamuzi huo umefanyika baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 6-0 dhidi Yanga ambapo viongozi wa timu hiyo waliamua kusitisha mkataba wa kocha huyo.
“Tunatambua na kuthamini jitihada walizofanya katika kuboresha utendaji wa timu yetu na tunamshukuru kwa mchango wake uliotukuka kwa kipindi chote alichoongoza timu yetu.Tunamtakia Kocha Mecky Maxime na wasaidizi wake kila la kheri,” ilieleza taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa Mbeya City FC.
Maxime anaondoka Mbeya City baada ya kudumu kwa takribani siku 130 ambazo ni sawa na miezi minne na siku tisa tangu alipotambulishwa Desemba 7, mwaka jana, alichukua nafasi ya Malale Hamsini.
Maxime ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Dodoma Jiji amewahi kuznoa timu za Ihefu (sasa Singida Black Stars) na Mtibwa Sugar.
Kocha huyo alisaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia Mbeya City maarufu Wagonga Nyundo wa Mbeya.
Wakati Maxime anatua Mbeya City, aliikuta timu hiyo inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imecheza mechi 10 na kukusanya alama nane.
Hata hivyo, Maxime hakuwa na matokeo mazuri kwani ameiacha Mbeya City ikishuka nafasi moja kutoka 12 hadi ikiangukia 13 na alama zake 17.
Kocha huyo alichangia pointi tisa katika mechi tisa alizoiongoza timu hiyo, ikiwa ni wastani wa kupata pointi moja kila mechi. Kwa jumla Mbeya City imecheza mechi 19 za Ligi Kuu Bara na kukusanya alama 17.
Mechi tisa alizoongoza Maxime ndani ya Mbeya City, timu hiyo imeshinda mbili dhidi ya TRA United (2-0) na KMC (3-2), huku sare ni tatu dhidi ya Pamba Jiji (1-1), Dodoma Jiji (1-1) na Azam (0-0), ikipoteza nne dhidi ya Mtibwa Sugar (2-1), Fountain Gate (1-0), Singida Black Stars (4-1) na Yanga (6-0).
Wakati Maxime akiondoka Mbeya City, msimu huu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara, imeshuhudiwa makocha 15 wakiachana na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo matokeo yasiyoridhisha au kupata kazi katika timu nyingine.





