Na ATHNATH MKIRAMWENI
SERIKALI inatarajia kutumia kiasi cha sh. bilioni 195.66 kujenga Bonde la Mto Msimbazi kuanzia Juni, mwaka huu.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, alisema fedha hizo zinatokana na mkopo kutoka Benki ya Dunia, mchango wa Serikali ya Hispania na ruzuku Serikali ya Uholanzi.
“Gharama za jumla za mradi wa ujenzi wa Bonde la Mto Msimbazi ni dola za Marekani milioni 260 sawa na sh. bilioni 195.66, fedha hizo zinatokana na mkopo kutoka Benki ya Dunia, mchango wa Serikali ya Hispania na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi,” alisema.
Profesa Shemdoe, alisema utekelezaji wa mradi huo, utafanywa na Kampuni za China Civil Engineering Construction, China Railway Construction Cooperation Harbour na Channel Engneering Bureau Group Limited kwa gharama ya sh. bilioni 195.66.
Alisema kazi zitakazofanyika ni ubomoaji nyumba zilizolipwa fidia, uhamishaji wa miundombinu ya huduma, uondoaji wa udongo na taka, upanuzi wa mto, uimarishaji wa kingo zake na upandaji miti na nyasi kulinda mazingira.
“Mradi huu ni wa kijasiri na wenye maono, utaleta matumaini mapya, fursa za ajira na kuboresha maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo, pia mradi huu ni wa kihistoria na utabadilisha kabisa taswira ya bonde la Msimbazi kutoka eneo hatarishi kuwa kitovu kipya cha uchumi na maendeleo,” alisema Shemdoe.
Alisema mradi huo ni wa kimkakati na umebeba maono ya muda mrefu ya kuboresha maisha ya wananchi, hususan wakazi wa maeneo yanayozunguka bonde la Msimbazi.
Alisema wazo la mradi huo, lilianza mwaka 2018 kufuatia mafuriko makubwa yaliyosababisha maafa katika bonde hilo hivyo juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimefanikisha kufikia hatua hiyo ya utekelezaji.
Alibainisha kuwa, mradi huo unatarajiwa kunusuru maisha ya wananchi kwa kuondoa makazi maeneo hatarishi kwa mafuriko, ambapo zaidi ya kaya 3,000, zitahamishwa na kulipwa fidia stahiki.
Pia, mradi huo, utatoa fursa mpya za kiuchumi kwa kutengeneza takribani hekta 57 za ardhi salama za makazi na shughuli za biashara.
Profesa Shemdoe, alisema mradi huo, utahusisha uboreshaji miundombinu muhimu ukiwemo ujenzi wa daraja jipya la Jangwani na karakana ya mabasi ya mwendokasi katika eneo la Ubungo Maziwa, hatua itakayorahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya jiji hilo.
Shemdoe alisema mradi huo, utakabiliwa na changamoto ikiwemo uhamishaji wa wafanyabiashara waliopo eneo la mradi, Soko la Kariakoo na wamiliki wa gereji, hivyo aliwataka viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanatafuta maeneo mbadala kulinda ustawi wa wananchi hao.
Aliwashukuru wadau waliofanikisha upatikanaji wa fedha hizo, akasisitiza kuwa ushirikiano huo, unaonesha imani waliyonayo katika maono ya serikali katika kuboresha miundombinu na maisha ya wananchi.
WAZIRI ULEGA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliutaja mradi huo kuwa ni hatua ya kihistoria itakayodumu kwa vizazi vingi na utekelezaji wake, utaandika ukurasa mpya wa maendeleo ya Dar es Salaam.
Alisema muda mrefu eneo hilo limekuwa chanzo cha changamoto kubwa kwa wakazi, lakini kupitia mradi huo, serikali inalenga kulibadilisha kuwa sehemu yenye thamani ya kiuchumi, kijamii na hata kivutio cha utalii ndani ya Jiji ya Dar es Salaam.
Ulega alionesha imani kuwa, mradi utafungua fursa mpya za kipekee, ikiwemo uwezekano wa kuendelezwa shughuli za utalii wa mijini kupitia miundombinu itakayojengwa kando ya mto huo.
Akizungumzia sekta ya barabara, Ulega alisema Tanzania, imepiga hatua kubwa tangu uhuru kwa kujenga mtandao mpana wa barabara za lami na vijijini na mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za viongozi mbalimbali kuanzia Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere hadi Rais wa Awamu ya Sita, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Ulega alisema maendeleo hayo, yataendelea kuimarishwa na utekelezaji wa miradi mikubwa kama wa Msimbazi.
MHANDISI SEFF
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, alisema mradi huo, unakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 260 zinazotokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (Dola milioni 200), Serikali ya Hispania (Dola za Marekani milioni 30) na Uholanzi euro milioni 30.
Mhandisi Seff, alisema hadi sasa serikali imelipa kiasi cha sh. bilioni 73.69 kama fidia kwa waathirika wa mradi wapatao 2,551 kupisha uendelezaji wa eneo la chini la bonde, kundi hilo ni la waathirika wa mafuriko.
“Kundi la pili ni la waathirika 314 wanaoathirika na ujenzi wa matuta kwa ajili ya maeneo salama ya makazi na biashara. Viwango vya fidia kwa kundi la pili vimepelekwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kupata idhini ya kufanya uthamini,”alisema.
Alisema muda wa utekelezaji mradi, unatarajiwa kuwa miezi 24 tangu mkataba utakapotimiza masharti ya kuanza, inakadiriwa masharti ya kuanza yatatekekelezwa ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.
Mhandisi Seff alisema mkataba unatarajiwa kuanza rasmi ifikapo Juni, mwaka 2026.
RC CHALAMILA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, utakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya mafuriko ambayo miaka mingi, imekuwa ikiathiri miundombinu na shughuli za kiuchumi jijini humo.
Alisema wakati wa mafuriko, barabara na madaraja muhimu, yalikuwa yakifungwa hali iliyosababisha athari za kiuchumi, hivyo ujenzi wake utakuwa suluhisho.
Chalamila alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa, ukiwemo mabilioni ya fedha katika madaraja ya Jangwani, Kigogo na maeneo mengine, unaonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuboresha usafiri na kuimarisha uchumi wa jiji hilo ambalo ni kitovu cha biashara nchini.
Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za serikali, hususan TARURA na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha miradi ya barabara na madaraja inatekelezwa kwa ufanisi.




