Na MWANDISHI MAALUMU, Msumbiji
TANZANIA inaandaa mpango wa kitaifa wa hatua za mapema za kujiandaa kukabiliana na ukame kwa maeneo yanayokabiliwa na janga hilo kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Mpango huo ni jitihada za kupunguza athari za janga hilo nchini hali inayoonesha dhamira ya serikali kuacha utaratibu wa kusubiri madhara yatokee ndipo ichukue hatua.
Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. Jim Yonazi, katika ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu hatua za mapema kabla ya majanga iliyofanyika Mei 25, 2026, mjini Maputo nchini Msumbiji.
Alisema ukame una madhara makubwa katika kilimo, mifugo, rasilimali za maji, usalama wa chakula, maisha ya wananchi, maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.
“Kwa sasa Tanzania inaendelea kuandaa mpango wa kitaifa wa hatua za mapema dhidi ya ukame kwa msaada wa WFP, kwa kutambua bado ni moja ya majanga makubwa yanayoathiri nchi yetu,†alisema Dk. Yonazi.
Alifafanua mpango huo utawezesha kuwepo mifumo imara ya tahadhari na utekelezaji wa hatua za mapema kabla majanga hayajatokea.
Dk. Yonazi alieleza Tanzania imechagua kujifunza kutoka Msumbiji kutokana na mafanikio yake katika kuanzisha na kutekeleza mifumo ya hatua za mapema dhidi ya majanga, hususan ukame, mafuriko na vimbunga.
Alisema kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika kwa kubadilishana uzoefu na mbinu bora, kujifunza mifumo ya uratibu wa taasisi, vigezo vya kuanzisha hatua za mapema pamoja na namna ya kugharimia hatua hizo.
Katibu mkuu huyo alieleza uzoefu huo utasaidia kuunganisha hatua za mapema ndani ya mifumo ya hifadhi ya jamii kuongeza ufanisi katika kukabiliana na majanga.
AUPONGEZA UBALOZI WA TANZANIA
Katika hatua nyingine, Dk. Yonazi ameupongeza ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji kwa namna unavyoendelea kutekeleza majukumu yake na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Alisema hayo jana alipotembelea ofisi hizo pamoja na ujumbe alioongozana nao kwa lengo la kushiriki katika ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu hatua za mapema kabla ya majanga.
Dk. Yonazi alizungumza na watumishi wa ubalozi huo na kupokea taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu iliyotolewa na Mwambata Fedha, Samson Marwa kwa niaba ya Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji aliyekuwa katika majukumu mengine.
“Ninawapongeza namna mnavyoendelea kuiwakilisha nchi yetu, ni vyema kuendelea kuangalia fursa zilizopo na kuzitangaza hususan za kiuchumi zitakazowavutia kuja kuwekeza Tanzania, niwasihi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu,†alisema Dk. Yonazi
Mwambata Fedha, Marwa aliahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuhakikisha jukumu la msingi la uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji linaendelea kuimarika kwa manufaa ya nchi hizo mbili.




