Na NASRA KITANA
NI wiki mbili pekee zimesalia kabla ya kushuhudia mtanange kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kila moja ikitamba mechi itakuwa ya kisasi na rekodi.
Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Septemba 16, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.,
Yanga imeifunga Simba mara tano mfululizo, mara nne katika mechi za Ligi Kuu kwa misimu miwili mfululizo na mchezo mmoja wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa, Agosti 8, mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa timu hizo, kila mmoja alitamba kufanya vyema kutokana na maandalizi aliyoyafanya.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids, amesema kuwa anajua mchezo utakuwa mgumu na wenye changamoto nyingi lakini anahitaji kuibuka kidedea na kulipa kisasi.
Amesema wamekuwa wakipoteza dhidi ya wapinzani wao mara kwa mara, hivyo hawataingia kinyonge kwani wanataka ushindi kwa namna yoyote.
Fadlu amesema ana imani na kikosi chake kuwa kitafanya vizuri na kulipa kisasi kwani hataki kuona timu yake inaendelea kufungwa na wapinzani wao.
“Ni mchezo mgumu kwetu na wenye ushindani mkubwa lakini safari hii hatutakubali kupoteza, tunahitaji kupata ushindi na kulipa kisasi, tunahitaji kushinda na kubeba taji hilo,” alisema Fadlu.
Naye Meneja wa kikosi cha Yanga, Walter Harrson alisema kuwa Kocha wao Romain Folz anaendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha timu inapata ushindi na kuendeleza rekodi walizoweka awali.
Amesema kuwa msimu huu hawataki masihara wanahitaji kubeba mataji yote wakianza na Ngao ya Jamii kwa kumfunga Simba.
“Furaha yetu sisi ni kuendeleza rekodi ambayo tumeiweka kwa kumfunga Simba kila tunapokutana naye, mwalimu anaendelea na mipango na ameshawasoma Simba, hivyo tuna imani ataingia na mbinu mbadala ili kuweza kupata ushindi,” amesema Walter.
Meneja huyo amesema kuwa timu yao inaendelea na maandalizi yake kuelekea katika mchezo huo muhimu wakiwa katika kambi yao ya Avic Town jijini Dar es Salaam.
Amesema anajua mchezo utakuwa mgumu na wenye upinzani, lakini wana imani ya kupata ushindi na kuendelea kuwapa burudani mashabiki wao.
Msimu uliopita, Yanga ilitwaa Ngao ya Jamii kwa kuichakaza Azam, mabao 4-1 yaliyofungwa na Prince Dube, Yoro Diaby aliyejifunga, Stephane Aziz Ki na Clement Mzize, huku bao la Azam likiwekwa kimiani na Feisal Salum ‘Fei Toto’ mechi ilipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.




