Na ESTA MALIBICHE,
Iringa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema maendeleo makubwa yaliyopo nchini ni uthibitisho wa uongozi mahiri uliofanywa na serikali chini uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Wasira aliyasema hayo mjini Iringa, wakati akizindua kampeni Jimbo la Iringa Mjini, iliyoambatana na kumnadi Mgombea wa Ubunge Jimbo la Iringa Mjini, kupitia CCM, Fadhir Ngahilo.
Akitaja baadhi ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025, katika Jimbo la Iringa Mjini, Wasira alisema kwa miaka mitano, CCM imefanikiwa kujenga shule mpya nne na madarasa 114 bila wananchi kuchangia chochote.
Alisema hatua hiyo, imechangia kwa kiasi kikubwa, kuongezeka ufaulu kutokana na wanafunzi kujifunza katika mazingira rafiki.
Pia, alieleza katika kipindi cha mitano, shule nne mpya za sekondari zilijengwa, zikiwa na vyumba vya madarasa 134.
Alisema serikali ya CCM, imetekeleza ilani yake kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, zahanati tatu zimejengwa, vituo vya afya vitatu na kuboresha hospitali, lengo likiwa kupunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata matibabu.
Alitaja mradi mwingine ya kisekta uliotekelezwa kipindi cha miaka mitano, ni maji ambayo hivi yanapatikana kwa uhakika.
Alisema matarajio ya CCM kupitia Ilani yake ya 2025-2030, imeweka mpango kabambe wa kujenga shule mpya za msingi na sekondari 22, zahanati saba.
JIMBONI KALENGA
Akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu Jimbo la Kalenga wilayani Iringa, Wasira alisema CCM kupitia Ilani yake ya mwaka 2025-2030, imeainishwa kulenga kuwakomboa mwananchi na kumwinua kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi katika sekta mbalimbali.
Katika mkutano huo, uliofanyika Kijiji cha Nzihi, Wasira alisema idadi kubwa ya Watanzania, pato lao linategemea kilimo, serikali itaanzisha vituo vya zana za kilimo.
Alitolea mfano maeneo mengine ambayo ardhi yake ni kame likiwemo Jimbo la Isimani, Wasira alisema kuwa, Ilani ya mwaka 2025-2030, itaendelea kuweka nguvu zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waweze kulima mara mbili kwa mwaka.
Wakati akimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, Wasira aliwapongeza wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo hilo, kumpitisha katika kura za maoni.




