Na WAANDISHI WETU,
Kigoma
MRATIBU na mwanachama wa ACT-Wazalendo mkoani Kigoma, Said Bakema, ametoboa siri ya kukihama chama hicho na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa muda mfupi aliyofanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan mkoani humo ndiyo sababu iliyomfanya kuhamia CCM.
Bakema alieleza hayo mkoani Kigoma katika mkutano wa kampeni za mgombea Urais CCM, Dk. Samia ambapo alisisitiza amejiunga Chama tawala kwa ridhaa yake.
“Ardhi hii ina kitovu cha wazazi wangu, nasimama kuwaambia kwa ridhaa yangu nimeamua kuachana na chama nilichokuwepo na kujiunga CCM mchana kweupe,”alisema Bakema.
Alisema chama alichotoka alikuwa mgombea ubunge jimbo la Kigoma Kusini mwaka 2015 huku 2020 akiwa mratibu wa Mkoa wa Kigoma katika uchaguzi mwaka huu.
“Leo nasema ACT kwaherini naingia CCM rasmi, sijashawishiwa na mtu yeyote, bali kilichonishawishi ni matokeo ya muda mfupi ambayo umeyafanya wewe (Dk. Samia), naachana na chama ambacho mtu akiamka na hasira siku hiyo wote mnakuwa na hasira au akiamka ana furaha mnakuwa na furaha wote,” alieleza.
Bakema alisema amehamia CCM sababu ni Chama kinachoendeshwa kitaasisi badala ya kufanya mambo kwa danadana.
“Nimekuja nikiwa najiamini nimeingia katika chama imara, kinachoendeshwa na mtu imara na tutafika mbali,”alisema Bakema.
Aliwaambia watanzania na wana-Kigoma, Dk. Samia ni mgombea urais wa CCM, ambaye siyo katika Tanzania tuu hata Afrika Mashariki ndiye mgombea anayekubalika.
“Nina faraja kujiunga chama kinachoongozwa na mtu mwenye maono makubwa ya kuwatumikia watanzania na mimi nataka niwatumikie watanzania. Kigoma umetusaidia sana katika kipindi kifupi, matokeo makubwa yameonekana,” alisema mratibu huyo.
Alitoa mfano Kigoma ilikuwa abiria akipanda basi saa moja jioni anafika Dar es Salaam saa moja jioni maana yake anatumia saa nyingi njiani kinyume na hivi sasa.
“Siko peke yangu nina watu wengi zaidi wapo tayari kunifuata ni matokeo ya kazi uliyofanya ningewaleta hapa kusingekuwa na sehemu ya kukaa, nitanya kazi usiku na mchana lengo langu ushindi utakaoupata na mimi niongeze asilimia kadhaa ya kura,” aliongeza Bakema.
Awali, Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Mongela alisema wameona waanze na Bakema, ambaye walikutana naye njiani walipokuwa wakienda katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Tuliona tupo katika mawindo tunatafuta tembo Oktoba 29, lakini tumekutana na mbogo njiani tukasema tuanze naye wakati tunaelekea huko mbele,” alibainisha Mongela.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi alisema Bakema ana wafuasi zaidi ya 200 ambao watakabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma.




