Na VICTOR MKUMBO
KIPA namba moja wa Simba, Moussa Camara amefanyiwa upasuaji wa goti na umekwenda vizuri.
Kipa huyo alifanyiwa upasuaji wa goti nchini Morocco ambapo anatarajiwa kukaa nje ya dimba kwa kipindi cha kati ya wiki nane hadi 10.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema Camara amefanyiwa upasuaji wa goti na imekwenda vizuri.
“Camara amefanyiwa upasuaji wa goti nchini Morocco na umekwenda vizuri, tunatarajia kumkosa katika kipindi kisichopungua wiki nane hadi 10.
“Tunawaomba Watanzania na mashabiki wa Simba kuendelea kumwombea dua kuhakikisha anarejea katika hali yake ya kawaida na kurudi katika majukumu yake ndani ya Simba,” alisema.
Ahmed alisema Camara alifanyiwa upasuaji wa goti na madaktari bingwa nchini Morocco.
“Tuna imani kipa wetu atarejea dimbani kwa wakati akiwa fiti baada ya kupona majeraha yanayomkabili,”alisema.
Meneja huyo alisisitiza Watanzania wanatakiwa kuendelea kumwombea kipa huyo kuhakikisha anapona kwa wakati na kurudi katika majukumu yake ya kawaida.
Camara alipata majeraha ya goti alipokuwa akiwania mpira langoni mwake katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), dhidi ya Gaborone United ya Botwana na kulazimika kutolewa nje.
Takwimu zinaonyesha Camara ameshacheza mechi 29 za CAFCL huku Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), akifikisha mechi 16.
Katika hatua nyingine, Ahmed alisema kwamba wachezaji wengine wote waliokuwa katika majukumu ya timu zao za taifa, tayari walisharipoti kambini na kuanza mazoezi na wenzao tangu juzi.
Alisisitiza wapinzani wao Petro Atletico ya Angola, walitarajiwa kuwasili jana jijini Dar es Salaam kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), utakaochezwa Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Wachezaji wote waliokuwa katika timu zao za taifa tayari wamesharipoti kambini na kwamba wapinzani wetu Petro Atletico walitarajiwa kuingia nchini leo (jana) kwa ndege ya kukodi,” alisema Ahmed.
Katika michuano ya CAFCL, Simba imepangwa kundi D ikiwa na timu za Petro Atletico ya Anngola, Stade Milien ya Mali na Esperance ya nchini Tunisia.




