Na NASRA KITANA
WAKATI Simba ikitarajiwa kuvaana na Petro de Luanda kesho, uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi wamewaomba mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuisapoti miamba hiyo.
Simba itachuana na Petro de Luanda saa 10:00 jioni katika mchezo wa kwanza wa kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Akizungumza Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema ni muhimu mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuhakikisha miamba hiyo inashinda kuanza vyema katika kundi hilo.
Ahmed amesema ili kupata matokeo mazuri, mashabiki wao wanatakiwa kuonyesha sapoti kubwa katika mchezo huo.
Amesema huo ni mchezo mgumu kwao kulingana na hatua ambayo wapo kwani hivi sasa kila timu inatafuta pointi tatu, hivyo wanapaswa kutumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri.
“Huu ni mchezo muhimu kwetu kwani tunahitaji kupata ushindi katika mchezo huu mgumu, hivyo mashabiki wanatakiwa kujaa kwa wingi kuwapa nguvu wachezaji wetu hasa tukiwa katika uwanja wetu wa Mkapa, mchezo wetu wenyewe na mashabiki wanajua furaha ipo katika ushindi hilo ni jukumu la wachezaji kutupambania mpaka mwisho,” amesema Ahmed.
Amesema lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanapata ushindi katika kila mchezo wa nyumbani na ugenini hivyo ni muhimu mashabiki kuwapa sapoti ya kutosha wachezaji wao ili kufanikisha.
Meneja huyo amesema hawana hofu na kikosi walichokuwa nacho kwani kila mmoja anajua umuhimu wa mchezo huo na wengi wao ni wazoefu katika mashindano hayo.
Katika hatua hiyo Simba imepangwa kundi D ikiwa na timu za timu za Esperance Sportive kutoka Tunisia, Petro De Luanda ya Angola na Stade Malien kutoka Mali.




