Na MWANDISHI WETU
UONGOZI wa Simba umetakiwa kuboresha safu ya ushambuliaji kuhakikisha inapata matokeo mazuri mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Keshokutwa, Simba itashuka dimbani ikiwa ugenini kupambana na Stade Malien ya Mali katika mchezo wa pili wa CAFCL hatua ya makundi.
Simba itaingia katika mchezo huo, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza bao 1-0 mbele ya Atletico Petro de Luanda, nyumbani, mechi ya kwanza hatua ya makundi iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Stade Malien ikilazimishwa suluhu ugenini dhidi ya Esperance Sportivo de Tunis ya Tunisia.
Simba ilianza michuano hiyo hatua ya awali msimu huu kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Gaborone United kabla ya sare ya 1-1 nyumbani, baadaye ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Nzingizi Hotspur kabla ya suluhu ya nyumbani.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa katika hatua ya awali ya kufuzu kucheza makundi ya CAFCL, Stade Malien ilishinda 5-0 dhidi ya Tempele Macaf kabla ya kuichakaza 2-0 ikiwa nyumbani.
Mechi za hatua ya kwanza, Malien ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Noudhibou mchezo wa marudiano ikishinda mabao 2-0.
Katika mechi ya kwanza hatua ya makundi, ikiwa ugenini Stade Malien ililazimishwa suluhu dhidi ya Esperance Sportivo de Tunis ya Tunisia.
Timu hiyo itaikaribisha Simba katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi utakaofanyika keshokutwa nchini Tunisia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wadau wa soka walisema Simba inatakiwa kufanya uboreshaji wa safu ya ushambuliaji kuhakikisha inafanya vyema kimataifa.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga, Charles Mkwasa alisema uongozi wa Simba unatakiwa kuboresha eneo la ushambuliaji kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mechi zitakazofuata.
Alisema Simba haikuwa na sababu ya msingi kupoteza mechi ya kwanza kwani walikuwa nyumbani na walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia vizuri.
Alisisitiza wachezaji wa Simba walikuwa wakipoteza mipira katika maeneo muhimu kitu.
“Simba walicheza mechi, lakini haikuwa sahihi wao kufungwa kutokana na umakini mdogo ndiyo maana walipoteza.
“Kiufundi walionekana wana udhaifu safu ya ushambuliaji ikiwemo kupoteza mipira katika sehemu muhimu kitu kilichowapa ugumu kupata ushindi huku wapinzani wakiwa na kasi hasa ya kushambulia.
“Uongozi unatakiwa kufanyia kazi kasoro hizo, hasa katika eneo la ushambuliaji, bado wana mechi nyingi kama wakibadilika wanaweza kufika mbali zaidi,” alisema.
Mchezaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema uongozi wa Simba unatakiwa kufanyia kazi upungufu uliyojitokeza katika mchezo wa kwanza hasa safu ya ushambuliaji.
Alisema Simba ilitengeneza nafasi nyingi lakini ilishindwa kuzitumia kutokana na washambuliaji wake kutokuwa makini kukwamisha mipira wavuni.
Alisema safu ya ushambuliaji inatakiwa kufanyiwa kazi kuhakikisha wanawajibika kufunga mabao mengi.
“Simba haikucheza katika kiwango ambacho wengi tulikitarajia tangu awali kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.
“Safu ya ushambuliaji inatakiwa kufanyiwakazi kuhakikisha timu inatumia nafasi nyingi wanazozitengeza na kupachika mabao,” alisema Mogella.
Wakati huo huo, uongozi wa timu hiyo umeweka wazi kuwa bado haujakata tamaa kwani wanajipanga kwa ajili ya mchezo unaofuata utakaopigwa Novemba 30, mwaka huu wakiwa ugenini.
Pambano hilo limepangwa kufanyika Stade Malien ya Mali mchezo utakaochezwa Uwanja wa 26 Mars.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa pamoja na kupoteza mchezo wa kwanza lakini bado hawajakata tamaa.
“Tumepoteza mchezo mmoja tu, ndio imetuumiza kwa kiasi kikubwa lakini hatujakata tamaa, tutapambana kuhakikisha tunashinda katika mechi zilizobakia za kundi letu,” alisema Ahmed.
Hata hivyo, Ahmed alisema kuwa timu yao inatarajiwa kuondoka jijini, Novemba 27 mwaka huu kwenda Mali kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao dhidi ya Stade Malien.
Alisema kuwa mwalimu ametaka timu yao isafiri mapema ili kwenda kurekebisha mapungufu yaliojitokeza katika mchezo wa kwanza.
Hadi sasa, Simba inaburuza mkia katika Kundi D linaloongozwa na Petro de Luanda, huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Espérance Sportive de Tunis yenye pointi moja, sawa na Stade Malien ya Mali.
Simba ipo kundi D ikiwa na timu za timu za Esperance Sportive kutoka Tunisia, Petro De Luanda ya Angola na Stade Malien kutoka Mali.




