Na REHEMA MOHAMED
MAHAKAMA Kuu Masijala Ndogo ya Dodoma, imemhukumu Augustino Amos, kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya Michael Mwimba.
Pia, Mahakama hiyo, imemwachia huru Emmanuel Ngosha na Emmanuel Molla kwa sababu, ushahidi haujatosha kuwatia hatiani.
Hukumu hiyo, ilisomwa mahakamani hapo na Jaji Evaristo Longopa, baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbali.
Washitakiwa hao, walidaiwa kutenda kosa hilo Februari 9, 2023 eneo la Shule ya Masingi Manyoni, Singida.
Ilidaiwa walimjeruhi Mwimba katika jicho la upande wa kushoto na nyuma ya kichwa.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ilimtia hatiani Amosi kwa sababu alikiri kutenda kosa kupitia maelezo yake ya ungamo.
Ilielezwa kuwa, kupitia maelezo hayo yaliyoandikwa kwa hiyari yake, mshitakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo.
Ilielezwa kuwa, maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, yalithibitishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba, kulikuwa na majeraha mawili makubwa katika mwili wa Mwimba, yaani sehemu ya nyuma ya kichwa na upande wa jicho la kushoto.
Katika maelezo hayo, mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo akishirikiana na mtu aliyemtaja kwa jina la Ndutu na Ngosha.
Alieleza walifanya hivyo baada ya kutumwa na mfanyabiashara Molla (mshitakiwa wa tatu), ambaye alikuwa akihitaji damu ya mzee.
Pia, ushahidi wa daktari na ripoti yake iliyopokelewa kama kielelezo namba moja, unaonesha kuwa, Mwimba alipata majeraha hayo ambayo yanalingana na maelezo yaliyomo katika maelezo ya onyo.
Kutokana na hali hiyo, mahakama iliona ushahidi unatosha kuthibitisha kwamba kulikuwa na kifo cha mtu kisicho cha kawaida, hivyo ilimtia hatiani na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.




