Na VICTOR MKUMBO
KOCHA wa timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Elieneza Nsanganzelu ametoboa siri ya kubeba ubingwa wa michuano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2026), Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ni maandalizi mazuri waliyofanya.
Serengeti Boys, ilitwaa ubingwa wa michuano ya CECAFA kufuatia kuichapa Uganda kwa mabao 3-2, katika fainali iliyofanyika Uwanja wa Abebe nchini Ethiopia.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa michuano ya CECAFA, Kocha Nsanganzelu alisema wamefanikiwa kutwaa ubingwa huo baada ya kupata muda mzuri wa kujiandaa.
“Tunashkuru Mungu kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya CECAFA msimu huu kwani haikuwa rahisi kutokana na upinzani tuliokutana nao.
“Siri kubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ni kufanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wangu walifuata maelekezo kwa kiasi kikubwa huku kila mmoja akitimiza majukumu yake uwanjani,” alisema kocha huyo.
Nsanganzelu alisema michuano ya CECAFA haikuwa rahisi, lakini walipambana kuhakikisha wanafanya vizuri ikiwemo kufuzu kucheza AFCON na kutwaa ubingwa.
Aliwapongeza wachezaji wake kutokana na kila mmoja kutimiza majukumu yake uwanjani na kwamba ana imani wataendelea kutunza kiwango kuhakikisha wanafikia malengo ya kubeba taji la AFCON 2026.
Pamoja na kutwaa ubingwa, timu hiyo ilibeba tuzo za Kocha Bora (Nsanganzelu), Mfungaji Bora (Luqman Mbalasalu) na Kipa Bora akiwa Haji Ally.
Nahodha wa Serengeti Boys, Kassim Selemani alisema walipambana kupata ushindi katika mechi zote kutokana na maandalizi mazuri waliyoyapata na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.
“Tumepambana kila mmoja kwa nafasi kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea na ubingwa huu siyo wetu wachezaji pekee bali ni kwa ajili ya Watanzania ambao wamekuwa mstari wa mbele kutupa sapoti tangu tunaanza michuano ya msimu huu.
“Tutaendelea kupambana kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa AFCON 2026 na kulileta kombe Tanzania,” alisema Selemani.
Katika michuano hiyo, Serengeti Boys iliandika historia kufuatia kushinda mechi zote msimu huu, Serengeti Boys ilianza michuano hiyo kwa kuichapa Sudan mabao 6-0, kabla ya kuirarua Djibouti idadi hiyo hiyo, iliifunga Burundi 5-0 na kutinga hatua ya nusu fainali.
Katika mchezo wa nusu fainali iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Kenya kabla ya kuishushia Uganda kipigo cha mabao 3-2 juzi.
Kufuatia matokeo hayo, Serengeti Boys imefuzu kucheza fainali za AFCON 2026 ikifuatana na Uganda na Ethiopia katika Ukanda wa CECAFA.




