Na NASRA KITANA
WACHEZAJI wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, wamepewa programu maalumu za mazoezi wanapokwenda nyumbani ili kulinda viwango vyao.
Ligi Kuu Tanzania Bara, imesimama kwa muda kupisha michuano ya Fainali yza Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON) 2025 inayotarajiwa kufanyika nchini Morocco.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa wachezaji ambao hawajaitwa katika timu za taifa ,wamepewa programu ya mazoezi ya asubuhi na jioni ili kuhakikisha hawaongezeki uzito.
“Mara nyingi wachezaji wakiwa katika mapumziko wamekuwa wakizembea kufanya mazoezi ,lakini safari hii mwalimu, Suleiman Matola amewapa kazi maalumu huku kila mmoja akitakiwa kuripoti katika makundi maalumu kujiweka fiti.
“Kila mchezaji amepewa programu yake maalumu kwa kipindi hiki ligi imesimama, mwalimu hataki masihara anataka kuona kila mchezaji akifanya mazoezi na kuonyesha kile ambacho amembiwa kufanya lakini pia wanatakiwa kuingia kumbi za mazoezi Gym kuweka miili yao sawa,” alisema Ahmed.
Hata hivyo, Ahmed alisema wachezaji ambao hawajaitwa katika kikosi cha timu ya Timu zao za Taifa wamepewa mapumziko hadi Desemba 28, mwaka huu ndio watarejea kambini.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa kocha wao, Pedro Goncalves amewapa programu maalumu wachezaji wake kuhakikisha wakiwa katika mapumziko hawatakiwa kubweteka.
Alisema kila mchezaji amepewa mazoezi ambayo anatakiwa kufanya lengo likiwa ni kurejea wakiwa imara na bora zaidi ya walivyokuwa mwanzo.
“Tunajua kutakuwa na mapumziko ya muda mrefu, lakini mwalimu wetu Pedro amempa kila mchezaji programu maalumu ya kufanya katika kipindi hiki cha mapumziko, mwalimu amesisitiza kila mmoja kufanya kile ambacho amemuagiza na atayepuuza basi adhabu kali itamkumba,” alisema.
Kamwe aliongeza kuwa timu imepewa mapumziko hadi Desemba 15, mwaka huu ambapo wataanza mazoezi hadi Desemba 20 na Desemba 21 watapumzika tena hadi Desemba 28 na Desemba 29, mwaka huu wachezaji wote wanatakiwa kurejea kambini,” alisema Kamwe.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano Azam FC, Zacharia Thabit ‘Zaka za Kazi’, alisema wachezaji wa timu yao wamepewa mapumziko hadi Desemba 22 mwaka huu ndio wataingia kambini kwa ajili ya programu zinazofuatia.
Alisema kuwa pamoja na mapumziko hayo lakini mwalimu Florent Ibenge amewapa mazoezi maalumu wachezaji wake kujiweka sawa.
“Timu ipo mapumziko, lakini mwalimu wetu amewapa mazoezi maalumu wachezaji wake ambapo kwa siku watafanya mazoezi asubuhi na mchana ili kuhakikisha wanarejea wakiwa fiti na bora kwa ajili ya kuendeleza mapambano,” alisema Zaka.




