Na MWANDISHI MAALUM
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ngwaru Maghembe, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyia leo Desemba 17, 2025.
Dk. Maghembe ameshiriki kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) katika kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao.
Kikao hicho kimefunguliwa na kuongozwa na Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Mwenyekiti wa Mpito wa Baraza la Mawaziri, Ronald Lamola, ambapo nchi wanachama zimejadili hali ya kisiasa na usalama katika Jamhuri ya Madagascar.
Aidha, Kikao kimepokea na kuridhia pendekezo la Jamhuri ya Zambia kushika nafasi ya Mwenyekiti Ajaye wa Mpito kufuatia Jamhuri ya Afrika Kusini kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Mpito wa SADC.
Mawaziri hao pia wamepitisha bajeti kwa ajili ya kuiwezesha SADC kutekeleza jitihada zake za kuisaidia Madagascar kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo.
Mkutano huo wa mawaziri umetanguliwa na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika asubuhi ya leo Desemba 17, 2025, ambapo Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dk. Samwel Shelukindo aliongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho.
Balozi Shelukindo ameungana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini akiwemo Naibu Katibu Mkuu wizarani, Balozi Said Shaib Mussa, pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania, Lut. Jen. Salum Haji Othman.




