LONDON, England
ARSENAL ya Mikel Arteta itasherehekea Sikukuu ya Krisimasi mwaka huu ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Wakati michuano hiyo ikielewa katikati mwa msimu, nini maana ya kuongoza ligi katika sikukuu hiyo hususan katika mbio za ubingwa?
Sikukuu ya Krisimasi husherehekewa Desemba 25 ya kila mwaka ikimaanisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Katika msimamo huo, Arsenal ndiyo kinara ikiwa na pointi 39 katika mechi 17 wakati Man City ikiwa nafasi ya pili kwa alama 37 baada ya kucheza mechi 37.
MBIO ZA UBINGWA
Timu ambayo huwa kileleni mwa msimamo katika Sikukuu ya Krisimasi mara nyingi huwa bingwa wa msimu husika, japokuwa siyo mara zote.
Katika misimu 33 iliyopita, timu 17 zilizoongoza ligi katika sikukuu hiyo, zilitwaa taji katika msimu huo.
Hata hivyo, Arsenal yenyewe imeshindwa kunufaika na jambo hilo kwani awali imeshakuwa kileleni mwa msimamo mara nne wakati wa Krisimasi lakini haijatwaa ubingwa.
Katika misimu 33 iliyopita, Man United (7) na Chelsea (5) ndizo timu zinazoongoza kwa kutwaa taji hilo mara nyingi (5) baada ya kuwa kileleni mwa msimamo katika Krisimasi wakati Liverpool ikifuatia kwa kutwaa mara mbili katika Krisimasi saba.
Kabla ya Mikel Arteta kuichukua timu hiyo, Arsenal iliwahi kuongoza katika Krisimasi mara mbili, lakini sasa ni mara ya tatu katika misimu minne ‘The Gunners’ inaongoza ligi Krisimasi.
Mashabiki wa Arsenal wanaamini kwamba kwa mara zote ambazo Arsenal imeongoza ligi katika Krisimasi na kushindwa kutwaa taji, basi imetosha na sasa Arteta ana kila sababu ya kuipa miamba hiyo kombe la kwanza la EPL ndani ya miaka 21.
ARSENAL INAWEZA KUFIKA MBALI?
Hakupaswi kuwa na sehemu yoyote ya kufanya makosa kwani miamba hiyo kutoka London hivi sasa inaongoza ligi kwa utofauti wa alama mbili pekee dhidi ya Man City wakati wastani wa timu bingwa kuongoza ligi katika Krisimasi ni pointi nne.
Kwa mujibu wa mchanganuo huo, timu pekee ambayo imeongoza ligi kwa alama chache katika Krisimasi ndani ya misimu 12 iliyopita ni Arsenal miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, Arsenal ndiyo timu pekee kushinda taji la EPL bila ya kufanya hivyo wakati inaongoza ligi katika Krisimasi, ambapo mataji yake yote matatu yaliyopita miamba hiyo haikuwa kinara katika Krisimasi.
Miamba hiyo iliwahi kuwa nyuma kwa alama 13 dhidi ya kinara Man United na ikaenda kutwaa taji la EPL msimu wa 1997/1998.
Pia, miamba hiyo ilikuwa nyuma pointi mbili dhidi ya Newcastle mwaka 2001/2002 na ikaenda kutwaa taji kabla ya kuwa nyuma kwa alama tatu dhidi ya Man United msimu wa 2003/2004 na ikaenda kubeba taji.
Arsenal itakuwa ya tofauti msimu huu?
Mashabiki wengi wa Arsenal wamezoea kuishuhudia timu yao ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England katika Krisimasi na baadaye kukosa taji hususan dhidi ya Man City ya Pep Guardiola.
“Tumerejea kileleni mwa msimamo lakini hatuitazami sana Man City au timu nyingine.,” alisema nyota wa Arsenal, Bukayo Saka.
Arteta alisema: “Tupo kileleni sasa, tunajua kama tutashinda kila wiki tutakaa palepale. Kitu pekee tunachoweza kilichopo katika uwezo wetu ni kiwango chetu binafsi na matokeo na tunajua ni kwa kiasi gani ligi ni ndefu na ngumu,”.
Hata hivyo, Kocha Pep Guardiola, alisema timu yake itaendelea kuwepo katika mbio za ubingwa huku akikisisitiza wanahitaji kuwa bora zaidi.




