NA JANE MIHANJI
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuielimisha jamii, juu ya faida za muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kuwarithisha vijana historia ya taifa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Hamad Yusuf Masauni, wakati wa semina kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, iliyolenga kutoa elimu juu ya wajibu wa vyombo vya habari katika kulinda na kuendeleza muungano.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dk. John Nchimbi, Waziri Masauni alisema ni wajibu wa vyombo vya habari kukuza uelewa na ufahamu wa historia ya taifa kwa vijana.
“Muungano wetu umedumu karibu nusu karne, lakini kuna vijana wengi hawajui historia wala faida ya muungano huu, hivyo ni wajibu wa waandishi wa habari kutoa elimu sahihi juu ya muungano huu ambao umekuwa kichocheo cha amani, mshikamano na utulivu miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Aliitaka jamii kuacha upotoshaji unaoweza kusababisha mgawanyiko na hivyo kuwataka wanahabari kuandika taarifa sahihi, zenye vyanzo vya uhakika, kuandaa makongamano na mijadala yenye tija kuzungumzia mafanikio ya muungano.
Masauni alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa vijana, kuhusu muungano kulinda historia ya taifa na kuwajenga katika uzalendo wa nchi yao.
Mapema akitoa mada kuhusu chimbuko, misingi na faida za Muungano, mwanasiasa mkongwe Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kizazi kipya cha uongozi na jamii ambayo haijashiriki au kuona nchi ilivyopata uhuru na muungano ni vema ikatambua thamani hiyo.
“Ni lazima historia ikawekwa kwa usahihi kwani madhara ya historia potofu ya nchi ni makubwa kwa vizazi na vizazi,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza kuwa asilimia 70 ya vijana walizaliwa baada ya muungano, hivyo wanapaswa kujua ukweli kuhusu muungano.
Kwa upande wake, mwanahabari nguli, Salvatory Rweyemamu akitoa mada kuhusu wajibu wa waandishi wa habari katika kulinda na kuuenzi muungano alisema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kuulinda muungano.
“Muwe waangalifu katika uandishi, uzalendo ni kitu muhimu sana, waandishi wa mataifa ya magharibi huwaoni hata siku moja wakizungumza kuhusu kuuvunja muungano wao, lakini wamekuwa wakiandika kuhusu mataifa mengine…hili ni la kujifunza,” alisema.
Aliwataka waandishi wa habari kupunguza ushabiki kwenye masuala ya muungano kwasababu hauna faida na badala yake mijadala inayoibuliwa iongozwe kwa kuwa na taarifa sahihi.
Sambamba na muungano, Rweyemamu alisisitiza pia kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar ambayo aliyataja kuwa ni mhimili mkuu wa Muungano.
Mafunzo hayo yamekuja huku muungano huo ukiwa na umri wa miaka 61 tangu kuasisiwa kwake Aprili 26, mwaka 1964.




