RABAT, Morocco
NYOTA wa timu ya taifa ya Morocco, Ayoub El Kaabi, juzi alinawiri kufuatia kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Zambia, katika mchezo wa makundi wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), uliofanyika Uwanja wa Prince Moulay Abdallah, Rabat, Morocco.
Kufuatia ushindi huo, Morocco imetinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo kufuatia kumaliza kileleni mwa msimamo wa kundi A, ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Mali yenye pointi tatu huku Comoro na Zambia zikifikisha pointi mbili kila mmoja katika mechi tatu zilizocheza.
Katika mchezo huo, El Kaabi alifunga bao la kwanza katika dakika ya tisa akiunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Azzadine Ounani na kuujaza mpira kimiani.
Morocco walionekana kulishambulia mara kwa mara lango la Zambia, dakika ya 27, ilipata bao la pili lililowekwa wavuni na mchezaji Brahim Diaz kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Abde Ezzalzouli.
El Kaabi alifunga bao la tatu dakika ya 50 kwa staili ya kibaiskeli pasi ya mwisho ilitoka kwa Ounahi na kuipeleka timu yake hatua ya 16 bora ya michuano hiyo msimu huu.
El Kaabi alisema, amefurahia kuisaidia timu yake kupata ushindi na kusonga mbele katika michuano hiyo huku wakimaliza hatua ya makundi wakiwa kileleni mwa msimamo.
“Tumemaliza hatua ya makundi ya michuano ya AFCON 2025 tukiwa kileleni, nimefurahia kuisaidia timu kutinga hatua inayofuata, tunakwenda kujipanga kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi mechi zijazo,” alisema.
Kufuatia ushindi huo, Morocco imetinga hatua ya 16 bora ikiungana na timu za Mali, Afrika Kusini, Misri, Nigeria na Algeria kabla ya mechi za jana.




