Hamis Shimye na
Hanifa Ramadhani
Zanzibar
UONGOZI wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, umeelezewa kutoa mwelekeo mpya wa mageuzi ya maendeleo, amani na utulivu kwa wananchi visiwani hapa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, kuhusu siku 100 za uongozi wa Rais Mwinyi tangu alipoapishwa kuongoza kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Nane, wawakilishi na wananchi mbalimbali walisema Zanzibar imesimama imara, imekuwa na mwelekeo thabiti wa kukua kiuchumi, kusonga mbele kutokana na utendaji kazi wake.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, alisema ndani ya siku 100 za uongozi, Rais Dk. Mwinyi, ameendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza chakula cha kuku na vifaranga, hatua inayotarajiwa kuimarisha sekta ya mifugo na kuongeza ajira.
Mbeto alisema katika kipindi hicho, kumefanyika uzinduzi wa kituo cha afya daraja la pili Kisiwa cha Tumbatu, mradi unaolenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
“Tunasema haya kwa ushahidi na takwimu. Ndani ya siku 100 kumefanyika kazi kubwa, yakiwemo maendeleo ya miundombinu ya masoko kama soko la Mwambasa na utekelezaji wa miradi mingine ya wananchi,” alisema Mbeto.
Mbeto alisema serikali inaendelea na mpango wa kuboresha usafiri wa umma, ambapo mabasi mapya ya kisasa yanatarajiwa kuanza kutumika.
Kuhusu usafiri wa majini, Mbeto alisema meli ya MV Mapinduzi ipo tayari inasubiri kukamilika taratibu za kibali ianze kutoa huduma kwa wananchi.
Alisisitiza serikali itaendelea kutoa taarifa na takwimu kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, ili wananchi wafuatilie maendeleo yanayofanyika.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walisema ndani ya siku 100, ameendelea kuimarisha umoja, mshikamano, amani na utulivu katika visiwa vya Zanzibar.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu wa Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, alisema Rais Dk.Mwinyi, ni kiongozi anayehubiri amani, umoja na maridhiano.
Alisema katika kipindi cha siku 100 za uongozi wake, amehakikisha amani inaendelea kuwa kipaumbele chake kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yoyote duniani.
“Tunashuhudia maendeleo ndani ya visiwa vyetu na hii inatokana na amani iliyopo Zanzibar,”alisema.
Alisema Rais Dk.Mwinyi, ameendelea kuimarisha huduma za jamii, miundombinu na kutekeleza miradi ya kimkakati.
Mwakilishi wa Jimbo la Kijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Badria Atai Masoud, alimpongeza Rais Dk.Mwinyi, kwa kasi yake ya maendeleo.
Alisema Rais Dk. Mwinyi alihakikisha anakamilisha daraja la ‘flyover’ la Mwanakwerekwe na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa daraja la pili la ‘flyover’ la Amani.
Alisema ‘flyover’ ya Amani inaendelea na hatua nzuri na ujenzi wake utakamilisha miezi michache baadaye huku ‘flyover’ ya Mwanakwerekwe ikiwa imefunguliwa.
Alisema miradi imekamilika kama bandari na barabara na mingine inaendelea kwa kasi na kusema dhamira ya Rais Dk. Mwinyi ni kubadilisha visiwa vya Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Chake chake, Abdulwahab Said Abubakar, alipongeza uongozi wa Rais Dk. Mwinyi, ni kiongozi mwenye maono makubwa.
Alisema Rais Dk. Mwinyi, amekamilisha miradi mikubwa kama ujio wa mabasi ya umeme jambo ambalo limekuwa faraja kwa wananchi.
Khatib Makame Faki, mkazi wa Paje alisema Rais Dk. Mwinyi ni alama ya mageuzi ya uchumi wa Zanzibar, kutokana na kazi kubwa aliyofanya ya kuleta maendeleo.
Alisema Zanzibar imekuwa kinara wa maendeleo na wananchi wanafanya biashara kwa uhuru na usalama.
Mwanasha Khamis Kambi, mkazi wa Ole, alisema Zanzibar imekuwa na mabadiliko ambapo maendeleo yaliyopo Pemba yamekuwa makubwa kuanzia bandari, uwanja wa ndege na Hospitali ya Abdallah Mzee kuna mabadiliko makubwa.
Februari 8, mwaka huu Rais Dk. Mwinyi, alitimiza siku 100 tangu aapishwe kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Novemba Mosi, mwaka jana kuanza kipindi cha pili cha Awamu ya Nane.
Sherehe za kuapishwa kwake zilifanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Jaji Khamis Ramadhan Abdallah, alimuapisha Rais Dk. Mwinyi baada ya kupata ushindi wa kishindo uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika ushindi huo, Rais Dk. Mwinyi alipata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 ya kura zote halali ambapo katika siku 100 za uongozi wake kumekuwepo na mafanikio makubwa ya uletaji maendeleo kwa wananchi.




