Na MWANDISHI WETU
UONGOZI wa klabu ya Yanga umetamba kuwa unakwenda kujenga uwanja wenye hadhi ya kimataifa ambao utatumika katika michuano mbalimbali na shughuli za kijamii.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa klabu hiyo, Hersi Said kupitia mtandao wa klabu hiyo kuwa wanakwenda kuweka historia kwa kujenga uwanja ambao utatumika katika majukumu mbalimbali ambayo yatasaidia jamii.
“Uwanja ambao tunakwenda kujenga utakuwa wenye hadhi ya kimataifa ndiyo maana tumefuata kanuni na sheria za CAF zinavyosema kipindi unataji uwanja uwe, pia tunakwenda kujenga uwanja ambao sio tu unahudumu mpira wa miguu pekee bali ni mradi ambao utakwenda kubeba majukumu mengine ya kijamii.
“Utakuwa na uwezo wa kutumika kwa lengo la hafla na shughuli mbalimbali,tunakwenda kujenga uwanja ambao unaakisi mandhari ya ubunifu utakaomudu mahitaji mbalimbali ya kijamii, sanaa, burudani na michezo,” alisema.
Rais huyo alisema mradi huo ni wa Yanga na GSM sio mali ya mtu bali ni mali ya taasisi hizo mbili.
“Mradi huu sio mali ya mtu bali ni mali ya taasisi hizi mbili Yanga na GSM, pia mradi utaendelea kujengwa iwe mimi ni Rais wa Yanga ama vinginevyo, GSM na Yanga wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika chini ya kiongozi yoyote ambaye atakuwa Rais wa Yanga.
“Nimejenga msingi bora na imara ambao utafanikisha jambo hili bila kumtegemea mtu, ikitokea mimi sio Rais wa Yanga, atakayechukua wadhifa huu anapaswa kujua analo jukumu la kuhakikisha ndoto ya ‘wananchi’ inatimia,” alisema.
Aidha, Hersi alisema wanatambua kiu ya mashabiki wao wanatamani kuona klabu yao ikiwa na kiwanja chao.
Aliwahakikishia wanachama, wapenzi, wadau wa Yanga kuwa wanakwenda kujenga uwanja bora na wa kisasa ambao utaweka historia nchini na nje ya mipaka yetu.
” Tunahitaji wiki moja kukamilisha mahitaji na malengo ambayo tumeafikiana leo, baada ya kikao cha pili kikao cha tatu tunakwenda kuweka historia GSM amesema siku anayosaini mkataba atahakikisha kazi inaanza mara moja, yupo tayari na anayo hamu kubwa ya kuanza na kukamilisha historia hii kubwa kwa klabu yetu,” alisema.
Rais huyo aliongeza kuwa wamejadili na kupitisha mchoro ambao wanahitaji kujengwa uwanja huo.
Pia,alisema wameridhia kwa pamoja kuwa mchoro huo umekidhi mahitaji yao na matakwa ya CAF.
“Tukishapata gharama zote za ujenzi wa kiwanja na tukaridhia, hatua ni ya mgawanyo wa majukumu na manufaa ya mradi huu kwa pande zote, kisha tunakwenda kusaini mkataba na mbia wetu GSM,” alisema.




