Na MWANDISHI MAALUMU, Kilimanjaro
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, amemtaka Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Reuben Kwagilwa, kufanya ufuatiliaji wa kina, kubaini iwapo kuna baadhi ya watendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA), wanaotumia kampuni zao binafsi kutekeleza miradi na kushindwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wake.
Dk. Mwigulu amesema haikubaliki kwa watendaji wa serikali kupokea fedha za utekelezaji wa miradi kisha kushindwa kuzitumia kwa wakati, hali inayosababisha wananchi kukosa huduma na maendeleo yaliyokusudiwa.
Dk. Mwigulu alitoa kauli hiyo, alipozungumza na wananchi wa Ndungu, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, ambapo ameanza ziara ya kikazi mkoani humo.
Alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akifanya jitihada kubwa kutafuta fedha kwa miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa watendaji kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa uadilifu na kwa wakati ili wananchi wanufaike.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu, alisema Rais Dk. Samia, ameelekeza kuwa, kila eneo halali la Mtanzania, lisichukukiwe bure kwa kuwa huo ndiyo urithi wake.
Pia, Waziri Mkuu, alikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Ndungu–Mkomazi yenye urefu wa kilometa 36 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mradi unaolenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.
Pia, Waziri Mkuu, aliziagiza serikali za vijiji, kuhakikisha wanazingatia matumizi bora ya ardhi.
“Kila mmoja aheshimu matumizi bora ya ardhi, wote wanaofanya kiburi tutashughulika nao, maana wanatupeleka katika kuondoa upendo miongoni mwetu,”alisema.
Dk. Mwigulu, jana alianza ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi wa changamoto mbalimbali.
Kabla ya kuingia Kilimanjaro, Dk. Mwigulu alianza ziara ya kikazi mkoani Tanga na kutembelea wilaya zote kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo tofauti.
Juzi, akiwa Lushoto, Mwigulu aliamuru baadhi ya mawaziri alioambatana nao, kubaki mkoani Tanga, kufuatilia masuala yaliyoibuliwa na wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Alitoa agizo hilo, alipozungumza na wakazi wa Soni na Bumbuli katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Soni, wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga.
Awakalia kooni DED, DC
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Same, kuhakikisha kiasi cha fedha sh. milioni 2.8 zinazodaiwa na mkandarasi aliyejenga vyoo, zinapatikana.
Mkandarasi huyo, aliwasilisha malalamiko hayo jana, katika mkutano wa wananchi mbele ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu.
Baada ya kusikiliza kilio cha mkandarasi, Dk. Mwigulu, aliamuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same….., Mkuu wa Wilaya hiyo,Kasilda Mgeni na wakuu wa idara, kuchangishana kiasi hicho papo hapo, kumlipa mkandarasi aliyejenga matundu ya vyoo 24 ya Shule ya Sekondari Gonjaseki.
Maagizo ya Waziri Mkuu, yaliibua shangwe kwa wananchi baada ya kutoa agizo hilo la kuchangishana fedha kutoka mifukoni mwao.
“Tangu mwaka 2022 hamjawahi kupata milioni mbili, sasa hapo mlipo hivi, toeni fedha mfukoni, nione mnamlipa hapa mkuu wa wilaya kaa pembeni na wataalamu wako ipatikane milioni mbili
“Halmashauri imekosa milioni mbili tangu mwaka 2022, mkurugenzi mapato yote mmekosa milioni mbili na matundu mnatumia?Hapa hapa nataka alipwe nataka aondoke na hela yake,”alisema.
Mkandarasi huyo, alisema alijenga vyoo vya shule mwaka 2022 bila kupewa malipo hadi kufikia jana.
Wakati huo huo, Dk. Mwigulu, alikerwa na kitendo cha mkazi wa Gonja, Mariaza Salim, ambaye eneo lake limechukuliwa na TANESCO kwa ujenzi wa kituo kidogo.
Mariaza, alisema baba yake alitoa bure eneo dogo kwa ujenzi wa kituo kidogo cha TANESCO Gonja, lakini shirika hilo liliongeza eneo jingine kwa ahadi ya kulipa fidia.
Alisema baada ya miaka 10, TANESCO walianza ujenzi mwingine kwa kuongeza eneo bila ridhaa yake, hatua iliyomfanya atoe malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, kudai haki yake bila mafanikio.
Baada ya kusikia kero ya Mariaza, Mwigulu, alimtaka ofisa wa TANESCO kutoa maelezo, ambapo ofisa huyo alikiri eneo hilo kuchukuliwa kwa makubaliano ya kumlipa fidia.
Alisema hataki kuona wananchi wakiteseka kwa makosa ya watendaji wa serikali ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao kwa wananchi.
“Mnapofanya tathimini mlipie mpaka lile mlilopewa bure, haya ndiyo mambo yanayoudhi wananchi
Mwanchi anajitolea eneo lake na eneo jingine mnachukua, eneo ndiyo utajiri analima ili apate chakula siyo mwajiriwa huyo,” alisema Dk. Mwigulu.




