Na WAANDISHI WETU
WAKATI michuano ya Ligi Kuu Bara ikizidi kunoga, kasi ya ukusanyaji wa pointi kwa timu nne kubwa katika mechi 11 za kwanza msimu huu imepungua, ukilinganisha na msimu uliopita.
Timu zilizocheza mechi 11 katika ligi hiyo msimu huu ni kinara Yanga, Simba (3), Azam FC (5) na Singida Black Stars nafasi ya tisa huku nyingine zilizobakia zikicheza kuanzia 13 hadi 17.
Timu hizo nne ambazo zimecheza mechi chache zaidi kutokana na ushiriki wake katika michuano ya kimataifa, msimu huu zimekuwa na kasi ndogo ya ukusanyaji wa alama katika mechi 11 za kwanza tofauti na ilizozikusanya msimu uliopita.
Licha ya kuongoza ligi kwa alama 29, Yanga msimu huu ina upungufu wa alama moja zaidi ya ilizokusanya msimu uliopita wakati Simba iliyopo nafasi ya tatu kwa pointi 24 ina upungufu wa pointi nne ya ilizokusanya msimu uliopita msimu uliopita.
Azam FC ambayo sasa ina pointi 23 katika nafasi ya tano ina upungufu wa alama moja ukilinganisha na msimu uliopita wakati Singida Black Stars iliyopo nafasi ya tisa kwa alama 19 ikiwa na upungufu wa pointi tano ukilinganisha na msimu uliopita.
Kwa mujibu wa takwimu, msimu uliopita katika mechi 11 za kwanza, Yanga ilikusanya alama 30, ikishinda 10 na kufungwa moja wakati Simba ikikusanya pointi 28 ikishinda tisa, sare moja na kufungwa moja.
Azam FC ilivuna pointi 24, ikishinda mechi saba, sare tatu na kufungwa moja sawa na Singida BS.
Msimu huu, Yanga imeshinda mechi tisa, sare mbili wakati Simba ikishinda mechi saba, sare mbili na kufungwa moja, Azam FC ikishinda mechi sita na sare tano huku Singida BS ikishinda michezo mitano, sare nne na kufungwa miwili.
Akizungumzia ushindani wa ligi hiyo msimu huu, aliyekuwa Kocha wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema michuano hiyo msimu huu ni migumu kwani kila timu inaonesha uwezo kuhakikisha inamaliza nafasi za juu.
Alisema baadhi ya timu ambazo hazijawahi kucheza michuano ya kimataifa zimekuwa na shauku ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao, hivyo zinapambana kuhakikisha zinamaliza nafasi nne za juu.
“Timu kama JKT Tanzania na Pamba Jiji zimekuwa na kiwango bora zaidi msimu huu na kwamba zinapambana kuhakikisha zinamaliza nafasi nne za juu ili kujihakikishia kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Ligi bado ni ngumu na kwamba hivi sasa huwezi kujua nani anayeweza kutwaa ubingwa msimu huu, lakini Simba na Yanga lazima zimalize nafasi ya kwanza na ya pili kutokana na uzoefu wao,” alisema Mkwasa.
Kocha na mchambuzi wa soka, Kenedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu imekuwa na ushindani wa aina yake.
Alisema michuano hiyo imeongeza ushindani baina ya timu kutokana na ubora wa timu zinazoshiriki msimu huu.
Alisisitiza timu zote zimekuwa katika ushindani wa hali ya juu kwani kila moja inataka kumaliza nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi na kufikia malengo waliyojiwekea.
“Ushindani ni wa hali ya juu zaidi msimu huu kwani kila timu inataka kumaliza katika nafasi nzuri na kufikia malengo iliyojiwekea.
“Ligi bado ni ngumu kila mmoja anamwomwombea mwenzake mabaya ili apoteze na kumpiku katika msimamo, hivyo bado ushindani utaendelea kuwa mkali zaidi katika mechi zitakazofuata,” alisema Mzazi.




