Dodoma
NA FRED ALFRED
TUME ya Ushindani (FCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaendelea na uchunguzi kuhusu gharama za bando zinazotozwa na kampuni za mitandao ya simu kubaini kama wananchi wanarubuniwa.
Hayo yalibainishwa jijini hapa na Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Khadija Ngasongwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali ya Awamu ya Sita ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Alisema uchunguzi utakaofanyika utatoa majawabu kama mlaji anaonewa au ni halali.
“Suala la bando za mitandao ni la kitaalamu ndiyo maana tuliona tufanye uchunguzi kwa kushirikiana na wenzetu wa TCRA ili tujue kama wananchi wanarubuniwa katika kupata huduma hizo,” alisema.
Aliongeza kuwa: ”Vilevile tunaendelea kushirikiana na Wakala wa Vipimo (WMA) kuangalia kiwango cha fedha kinachotozwa kinaendana na huduma anayopata ili kuthibitisha hayo kunahitaji uchunguzi wa kisayansi.”
BIDHAA BANDIA
Kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia Khadija alisema FCC imeendelea kusimamia kikamilifu Sheria ya Alama za Bidhaa ambayo jukumu muhimu katika kuzuia uingizaji,
uuzaji na usambazaji wa bidhaa bandia au zile zenye maelezo potofu.
Alisema bidhaa bandia huzuia ushindani wa haki, kuathiri vibaya biashara halali na kuhadaa watumiaji, hivyo kuunda uwanja usio sawa wa biashara.
“Sheria hii inahakikisha kuwa biashara zinapewa fursa ya kufanikiwa kutokana na ubora, ubunifu na kufuata sheria, badala ya udanganyifu. Hii inakuza soko lenye ushindani wa haki na uwazi, likilinda imani ya watumiaji na kuwezesha makampuni kuwekeza kwa kujiamini katika ukuaji na ubunifu,” alisema.
Aliongeza kuwa:”Kudhibiti bidhaa bandia kwa mujibu wa sheria hii pia kunachangia ukuaji wa uchumi. Biashara halali zinabaki na mapato yake, jambo linalochochea uwekezaji zaidi, kuongeza ajira na kuendeleza ubunifu.”
Alisema jitihada za kuzuia bidhaa bandia zinaboresha sifa ya biashara kitaifa na kimataifa, kuwavutia wawekezaji na kuongeza mauzo ya nje.
“Kwa kuunganisha utekelezaji madhubuti, ushirikiano wa sekta, na uhamasishaji wa umma, sheria hii inahakikisha kuwa ushindani wa haki na uthabiti wa kisheria unachochea ukuaji wa uchumi endelevu wa nchi,” alisema.
KUMLINDA MTUMIAJI
Khadija alisema FCC imepanga kuendeleza juhudi za kumlinda mlaji dhidi ya mienendo potofu, hadaifu na kandamizi katika soko la bidhaa na huduma na kudhibiti bidhaa bandia.
Alisema katika kutekeleza hilo imeendelea kutatua malalamiko ya walaji, ambapo katika robo ya kwanza na ya pili malalamiko 63 yalishughulikiwa, kati ya malalamiko hayo 45 yalipatiwa ufumbuzi 19 yaliyobaki yapo katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Pia alisema FCC ilisajili na kuthibitisha mikataba 27 inayoandaliwa na upande mmoja (SFCC), sanjari na kuandaa warsha na makongamano mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha inajenga uelewa kuhusu masuala ya kumlinda mlaji kwa wadau na mahusiano.




