Na MWANDISHI WETU
SERIKALI chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kuimarisha miundombinu na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali ya Tanzania.
Akizungumza katika futari maalumu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Khamis Omar amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kuhakikisha wanaimarisha miundombinu na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali nchini.
Wazir Omar alisisitiza kuwa serikali pia imekuwa na ushirikiano mzuri na Kampuni ya Airtel ambapo inamiliki hisa kwa asilimia 49 katika kampuni hiyo.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kuimarisha miundombinu na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali ya Tanzania,” amesema.
Waziri Omar, amesema kampuni hiyo inatakuwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Amebainisha kwamba sekta ya mawasiliano ina nafasi muhimu katika kuunda fursa za ajira, kusaidia shughuli za biashara na kuchangia mapato ya serikali.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel, Charles Kamoto alisema futari hiyo ilikuwa maalumu kwa viongozi wa serikali na wadau mbalimbali ikiwa na lengo la kuwaweka katika hali ya umoja, kutafakari na kutoa shukrani wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadani.
Amesema anawashukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao na kwamba ana imani futari hiyo imekuwa nafasi muhimu ya kuwakutanisha pamoja ikiwemo kubadilishana mawazo.
“Ramadani wakati wa kutafakari, kujitolea na mshikamano, tunashukuru kushiriki wakati huu maalumu na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali wanaendelea kutusaidia katika safari yetu ya kuunganisha Tanzania,” amesema.




