Na Mwandishi Wetu
MFANYABIASHARA na Rais wa heshima wa Simba Mohamed Dewji Mo, amezidi kuchomoza kimataifa baada ya kutajwa kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki na Kati.
Kuchomoza kwa Mo kumekuja kipindi ambacho serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ikiweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara kuvutia wawekezaji.
Katika kuthibitisha hilo, Jarida la Forbes limemtaja Mo kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 2.1.
Katika orodha hiyo, Mo amechomoza kwa kuifanya Tanzania kuongoza mabilionea kwa eneo zima la Afrika Mashariki na Kati.
Mo amechomoza katika orodha hiyo miongoni mwa bilionea vijana Afrika, kwa mujibu wa Jarida hilo la Forbes.
Kuchomoza kwa Mo ni sifa kwa Tanzania, kwani amekuwa akifanya biashara nyingi zikiwemo za vyakula, usafirishaji huku akitoa ajira, misaada ya kijamii ukiwemo ufadhili wa wanafunzi kupitia Mo Dewji Foundation, kulipa kodi na kuendesha Klabu kubwa ya Simba.
Chini ya Mo, Simba imekuwa ikipata mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa hivyo pia, kuitangaza nchi.
Katika orodha hiyo ya mabilionea, Ariko Dangote anaongoza Afrima kwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 28.5.




