Na NASRA KITANA
KOCHA wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi ameita kikosi cha wachezaji 25 akiwemo kipa wa Azam FC, Aishi Manula.
Gamondi raia wa Argentina amekiita kikosi hicho kwa mechi maalumu za kirafiki za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA Series) zitakazochezwa nchini Rwanda kuanzia Machi 26 hadi 29, mwaka huu.
Katika kalenda hiyo, Taifa Stars itachuana na Liechtenstein na Aruba au Macau.
Akitangaza kikosi hicho jijini Dar es Salaam, Gamondi alisema anaamini kikosi alichokiita kitakwenda kufanya vyema katika mechi hizo.
Gamondi alisema kwake siku zote hakuna mechi ya kirafiki anapenda kushinda kila mchezo.
“Siku zote kwangu mimi hakuna mchezo wa kirafiki, kila mchezo kwangu ni kama fainali, tunahitaji kupata ushindi katika kila mchezo ili tuweze kuimarika zaidi na kuw bora,” alisema Gamondi.
Wachezaji aliowaita kocha huyo ni Manula (Azam FC), Yona Amosi (Pamba Jiji), Zuberi Foba (Azam FC), Mohamed Mussa (Mashujaa Fc), Twalib Nuru (Azam FC), Bakari Msimu (Coastal Union), Elias Lameck (Azam FC) Haji Mnoga (Salford City, Uingereza) Nickson Kibabage (Simba SC) .
Wengine ni Bakari Mwamnyeto (Yanga) Mohamed Hussein (Yanga) Ibrahim Abdulla’Bacca’ (Yanga) Yusuph Kagoma (Simba), Kelvin Nashon (Pamba Jiji), Mudathir Yahya (Yanga), Novatus Dismas (Göztepe, Uturuki) na Alphonce Mabula (Shamakhi, Azerbaijan).
Wachezaji wengine ni Feisal Salum (Azam FC, Saimon Msuva (Al-Talaba, Iraq), Kelvin John (Aalborg Bk, Denmark), Iddi Suleiman (Azam FC), Charles M’mombwa (Floriana FC, Malta), Tarryn Allarakhia (Rochdale AFC, Uingereza), Paul Peter (JKT Tanzania) na Suleiman Mwalimu (Simba).




