Na ELIZABETH JOHN
BAADHI ya wasomi nchini wamesema wana imani kubwa na Tume Huru ya Kuchunguza Vurugu za Oktoba 29, mwaka jana, iliyoundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa wasomi hao, uwezo, uzoefu na weledi wa wajumbe wa tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Mohamed Chande Othman ambaye ni jaji mkuu mstaafu, utasaidia kubaini chanzo cha matatizo na kutoa mapendekezo sahihi ya namna ya kuyatatua.
Pia, wamesema amani na utulivu ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na ustawi wa mtu mmoja mmoja, wakisisitiza bila mazingira hayo, uzalishaji hauwezi kufanyika kwa ufanisi.
Novemba 8, mwaka jana, Rais Dk. Samia alitangaza rasmi kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka jana. Chini ya Jaji Chande, tume hiyo ina wajumbe saba.
DK. EMMANUEL KWAYU
Akizungumza na UHURU, Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Dk.Emmanuel Kwayu, alisema matarajio yake ni kuona tume ikija na majibu ya kina yatakayosaidia siyo tu kuelewa chanzo cha vurugu hizo, pia kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia matukio hayo kujirudia.
Amesema matokeo ya uchunguzi huo yakitekelezwa ipasavyo, yataimarisha utulivu wa kijamii na kisiasa, hali itakayochochea shughuli za kiuchumi kuendelea kwa ufanisi, hivyo kunufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia matukio ya vurugu za Oktoba 29, Dk. Kwayu amesema yaliathiri kiasi kikubwa uchumi, ambapo shughuli nyingi zilisimama na kusababisha hasara kwa wananchi na taifa.
“Miundombinu iliharibiwa ikiwemo vituo vya mabasi ya mwendokasi, vituo vya polisi viliharibiwa, hali iliyosababisha matumizi makubwa ya fedha za kukarabati,” amesema.
Dk. Kwayu amesema fedha zinazotumika kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa zingetumika katika shughuli nyingine za maendeleo, lakini kutokana na vurugu hizo, fedha zimetumika mara mbili kufanyia kitu kilekile, hali hiyo inarudisha nyuma jitihada za kukuza uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Mhadhiri huyo amesema amani na utulivu ni msingi muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na hata kwa mtu mmoja mmoja, akisisitiza bila hali hiyo, uzalishaji hauwezi kufanyika kwa ufanisi.
Amesisitiza mazingira ya utulivu huwapa watu nafasi ya kufanya kazi kwa bidii na kuongeza kipato, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
“Sekta binafsi na serikali haziwezi kufanikisha malengo ya uzalishaji endapo hakuna amani, uwekezaji na shughuli za kiuchumi hutegemea sana mazingira salama, wawekezaji huhitaji usalama kuendesha shughuli zao bila hofu ya vurugu au uharibifu wa mali,” amesema Dk. Kwayu.
PROFESA MJEMA
Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Emmanuel Mjema, alisema kutokana na tume hiyo kuundwa na watu wenye heshima, anaamini haiwezi kusema uongo hivyo wananchi wanapaswa kusubiri.
Alisema uzoefu wa wajumbe hao katika nyanja mbalimbali unawapa uwezo mpana wa kuchambua chanzo cha vurugu hizo kwa mitazamo tofauti na kutoa mapendekezo yatakayokuwa na tija kwa taifa.
Profesa Mjema alisisitiza endapo tume hiyo itapewa ushirikiano wa kutosha na wananchi pamoja na taasisi husika, ina uwezo wa kuja na suluhisho la kudumu litakalosaidia kuimarisha amani, mshikamano na maendeleo ya kiuchumi nchini.
Aidha, alisema amani ni nguzo kuu ya maendeleo ya kiuchumi kwa taifa lolote, akieleza bila utulivu wa kisiasa na kijamii, shughuli za uzalishaji na biashara haziwezi kufanyika vyema.
Profesa huyo alieleza mazingira ya amani huwapa wafanyabiashara na wawekezaji uhakika wa kuendesha shughuli zao bila hofu, jambo linalochochea ukuaji uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Alisema kunapokuwa na vurugu au migogoro, uchumi huathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kupungua uzalishaji, kuharibika miundombinu na kupotea fursa za uwekezaji.
“Hali hiyo husababisha pia kushuka mapato ya serikali, hivyo kudhoofisha utoaji huduma muhimu kwa wananchi kama afya, elimu na maji,” aliongeza Profesa Mjema.
DK. DANINGA
Mhandiri katika Idara ya Uongozi, Maadili na Utawala wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga, alisema anaamini wajumbe wa tume hiyo wamechaguliwa kwa kuzingatia uadilifu, taaluma na uzoefu unaohitajika katika kushughulikia masuala nyeti ya kitaifa.
Alifafanua mchanganyiko wa kitaaluma kwa wajumbe wa tume hiyo, unaipa uwezo wa kuchambua kwa kina kiini cha matukio hayo na kutoa mapendekezo yatakayokuwa na manufaa ya muda mfupi na mrefu.
Dk. Daninga aliongeza tume hiyo ina nafasi muhimu katika kuimarisha misingi ya utawala bora, haki na uwajibikaji nchini, akisisitiza matokeo ya kazi yake yataongeza imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.
Alisema ana matumaini mapendekezo yatakayotolewa yatasaidia siyo tu kudhibiti vitendo vya vurugu, pia kujenga mazingira ya amani, mshikamano na maendeleo endelevu ya taifa.
Pia, alisema kulinda na kudumisha amani inapaswa kuwa jukumu la kila mwananchi pamoja na taasisi za umma na binafsi, akibainisha mshikamano wa kijamii na utawala bora ni misingi muhimu ya kuhakikisha utulivu unaendelea kudumu.
Alisema taifa lenye amani lina nafasi kubwa zaidi ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, hali inayochochea ukuaji endelevu wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
MTAALAMU WA UCHUMI
Ladslaud Sillydion ambaye ni mtaalamu wa uchumi alisema amani ni kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi, kwani huweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, biashara na uzalishaji.
Alisema bila amani, shughuli nyingi za kiuchumi hukwama na kusababisha hasara kwa taifa na wananchi, ambapo ni muhimu utulivu kudumishwa wakati wote kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu.
WAJUMBE WA TUME
Pamoja na Jaji Chande, wajumbe wengine ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, IGP mstaafu, Said Mwema, Dk. Stargomena Tax, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Paul Meela, ambaye ni mwanadiplomasia na Luteni Jenerali wa Jeshi mstaaafu.
Novemba 20, mwaka jana, Rais Dk. Samia, aliizindua tume hiyo na kuipa siku 90 za kufanya uchunguzi huo hadi Februari 20, mwaka huu.
Aidha, Februari 21, mwaka huu, tume iliongezewa muda wa siku 42, huku taarifa ya uchunguzi ikitarajiwa kuwasilishwa Aprili 3, mwaka huu.
MJUMBE MAALUMU
Machi 11, mwaka huu, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Parfait Onanga-Anyanga, alikutana na Rais Dk. Samia alipowasilisha salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.
Onanga-Anyanga alisema umoja huo unatambua na kupongeza hatua zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania, baada ya matukio ya Oktoba 29, mwaka jana.
Alipongeza uamuzi wa kuundwa tume hiyo na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa pamoja na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya kikatiba.
Mjumbe huyo alikuwepo nchini kusikiliza maoni ya wadau na kutathmini hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani ya kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka jana.
Onanga-Anyanga aliongeza, UN inaendelea kuitambua Tanzania ni nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa na kuthamini mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani barani Afrika.
Vilevile, mjumbe huyo wa UN alikutana na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.
Kwa upande mwingine, alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi na wadau wengine wa kisiasa, kijamii kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu masuala vurugu zilizotokea na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali.
Onanga-Anyanga alibainisha ushirikiano huo utawezesha UN kupata taswira halisi kuhusu matukio ya Oktoba 29 na jitihada zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto zilizojitokeza.
SALAMU ZA RAIS DK. SAMIA
Rais Dk. Samia alituma salamu za shukrani na kupongeza hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres ya kutuma ujumbe maalumu nchini Tanzania kupata uelewa wa kina kuhusu hali ya nchi na kusikiliza maoni ya wadau.
Kupitia salamu hizo, alisema serikali imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio hayo unafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki, ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa ambao umekuwa msingi wa maendeleo ya nchi.
Rais Dk. Samia aliongeza serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume ya Uchunguzi baada ya kukamilisha kazi yake, kwani mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kuimarisha maridhiano ya kitaifa, pamoja na marekebisho ya katiba.
Alisisitiza Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na jumuiya za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi.




