AMINA KASHEBA
BONDIA nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo ameomba radhi kwa mashabiki wake kufuatia kupoteza pambano la kuwania mkanda wa Ubingwa wa Dunia (IBO) dhidi ya Michel Soro kutoka Ufaransa.
Mwakinyo alishindwa kutwaa mkanda huo baada ya kupoteza kwa Technical Knockout (TKO) katika raundi ya tisa ya pambano la raundi 12, uzito wa kati ambalo lilitarajiwa kuwa moja ya mapambano makubwa katika safari yake ya ngumi za kulipwa, lililofanyika nchini Ivory Coast.
Akizungumza baada ya kumalizika pambano hilo, Mwakinyo alitoa pole kwa mashabiki wote walioumizwa na matokeo hayo, kwani kushinda na kushindwa ni sehemu ya mchezo.
Alisema kilichomuumiza zaidi si kupoteza pambano hilo, bali kushindwa kuonyesha kiwango chake halisi kutokana na kuwa katika hali ya udhaifu ambayo ilimfanya ashindwe kujitetea ipasavyo ulingoni.
“Siuumii kwa sababu ni mchezo, lakini kinachoniumiza ni kuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kuonyesha upiganaji wangu wa kawaida, hiyo ndiyo sababu kubwa ya masikitiko yangu,” alisema Mwakinyo.
Mwakinyo alisema maandalizi yake yalikuwa mazuri na alifanya mazoezi makali ya nguvu kwa lengo la kuhakikisha anapata ushindi, lakini hali ya mwili wake siku ya pambano haikuruhusu kutoa kile ambacho mashabiki wamezoea kukiona kutoka kwake.
“Nimeyapokea matokeo haya narudi kujipanga upya kwani nitakuwa nipo imara zaidi katika mapambano yajayo, “ alisema Mwakinyo.
Matokeo hayo yanaifanya rekodi ya Mwakinyo kupata pigo jingine katika ngumi za kulipwa, huku Soro akiendelea kuthibitisha ubora wake katika medani ya kimataifa.
Wadau wafunguka
Promota wa ngumi za kulipwa, Ernest Evarist ‘Mopao’ alisema bado Mwakinyo ana muda wa kurekebisha kasoro zilizojitokeza kabla ya kupanda ulingoni katika mapambano mengine.
“Muda bado upo wa kufanya uboreshaji nina imani Mwakinyo ana nafasi ya kuonyesha uwezo wake, watanzania wanapaswa kufahamu mchezo wa ngumi una matokeo matatu,” alisema.
Bondia, Twaha Kassim ‘Twaha Kiduku’ alimpa pole Mwakinyo na kumtaka ajipange upya kwa ajili ya kufanya vyema katika mapambano mengine.
“Pole kwa Mwakinyo kwa kupoteza hili siyo jambo geni kwani utokea kwa mtu yoyote, muhimu anapaswa kujipanga upya na kuangalia wapo ameanguka,” alisema Twaha Kiduku.
Naye bondia, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ alisema matokeo ya juzi hayawezi kushusha kiwango na juhudi za Mwakinyo hivyo ana imani atafanya vyema wakati mwingine.
“Ninaamini bado una uwezo mkubwa, matokeo ya leo hayawezi kufuta juhudi na kipaji chako wapongeza wote waliocheza leo wameonesha mchezo mzuri japo bahati haikuwa kwetu,” alisema Dullah Mbabe.




