Na SIMON NYALOBI
MKUU wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere(MJNLS), iliyopo wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, Profesa Marcellina Chijoriga, amesema amani ni tunu inayopaswa kuenziwa na Watanzania wote kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo.
Profesa Chijoriga, alisema hayo, alipozungumza na UHURU na kwamba wananchi wanapaswa kulifahamu hilo katika maisha yao ya kila siku.
“Ukiwa na amani mambo mengi yanawezekana na bila ya amani hakuna maendeleo, tukumbuke amani inaanzia kwa mtu binafsi, jamii na baadaye kwa taifa kwa ujumla.
“Hivi sasa hapa nchini tuna miradi mikubwa ya maendeleo ya kitaifa, iwe katika barabara, maji na umeme, miradi yote hii inafanyika kwa sababu nchi ina amani, sasa ukienda katika nchi zenye vita huwezi kukuta miradi ya maendeleo inafanyika,”alisema.
KUENDELEZA AMANI
Akizungumzia mambo yanayoweza kuimarisha na kuendeleza amani, aliweka wazi kuwa ni muhimu kuwepo kwa umoja na mshikamano ndani ya taifa.
“Ili amani iwepo ni lazima umoja na mshikamano utamalaki, kusiwe na chokochoko za kuleta mifarakano na hata Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alisisitiza taifa liwe na umoja na mimi naongeza la kwangu upendo lazima uwepo,”alisema.
Profesa Chijoriga alisema tofauti za watu katika itikadi za vyama vya siasa au dini au tofauti za makabila hazina shida, lakini itikadi hizo zitakuwa na shida iwapo itikadi hizo zitakuwa zinachochea kutokea kwa mifarakano ndani ya jamii.
Alisisitiza mitizamo ya kisiasa isifanye watu wafarakane na kuvunja amani na umoja wa kitaifa, kwa kuwa nchi imejengwa katika misingi ya amani na umoja.
Profesa Chijoriga alisema viongozi wanaohubiri chuki na mifarakano hawafai na dhamira zao zisipewe nafasi katika taifa; kwa kuwa zitavunja amani na utulivu uliopo.
“Watanzania tuogope mifarakano ya aina yoyote inayotugawa katika umoja wetu, tumeshajengewa misingi mizuri na waasisi wetu; kwa mfano mimi ni mwenyeji wa Songea lakini niliolewa na mtu wa Musoma, hii ni tofauti na mataifa mengine watu wanaulizana makabila ndipo waamue waoane,”alisema.
Profesa Chijoriga alikumbusha msingi wa amani na umoja wa taifa wa nchi ulijengwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ambao uliwaunganisha wananchi wote na matumizi ya Lugha adhimu ya Kiswahili.
Kuhusu namna raia wa kigeni wanavyoichukulia amani na umoja uliopo nchini, alisema raia hao hususan wanaokwenda kusoma katika Shule ya MJNLS wanastaajabu fahari ya amani iliyopo nchini.
“Wageni wanaosoma katika shule yetu wanashangaa amani iliyopo na maendeleo tuliofikia, wageni hao ni wale waliotoka katika vyama vilivyopigania ukombozi wa Kusini mwa Bara la Afrika.
“Wanashangaa namna tunavyoendesha mambo yetu katika kuleta amani kupitia tume tunazounda wenyewe ikiwemo, Tume ya Uchunguzi kuhusu matukio ya machafuko wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025,” alisema.
Aliweka wazi kuwa, wanashanga kuona jitihada zinazofanywa na serikali katika kuleta utulivu na amani nchini ni tofauti na nchi zao.
Profesa Chijoriga akizungumzia kutokuwepo kwa ubaguzi katika masuala ya maendeleo ya umma hususan usafiri wa umma, alisema raia hao wa kigeni wanashangazwa na maendeleo yanayoletwa na serikali yanayogusa kila raia wa nchi.
Alifafanua, raia hao wa kigeni wamekuwa wakishangaa namna raia yeyote kutumia usafiri wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na usafiri wa treni inayotumia Reli ya Kisasa(SGR) bila ya ubaguzi.
Kwa mujibu wa Profesa Chijoriga, kushangaa kwao huko kunatokana na baadhi ya nchi zao ambako usafiri wa aina hiyo unafanyika kwa matabaka, kwani si kila mtu anayeweza kufurahia huduma ya usafiri wa aina hiyo.




