NA MUSSA YUSUPH
KATIKA historia ya Afrika hakuna jambo lililoathiri maendeleo yake kwa kina kama ukosefu wa Amani. Amani siyo tu hali ya kutokuwepo kwa vita, bali ni mazingira ya ukosefu utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kijamii na uhakika wa usalama kwa raia.
Pale ambapo amani imetamalaki, maendeleo yameonekana na pale ilipovunjika, umasikini, machafuko na mateso yamechukua nafasi.
Afrika imewahi kushuhudia migogoro iliyochukua maelfu ya maisha na kuiacha jamii katika majonzi makubwa. Nchi zilizokumbwa na vita vya muda mrefu zilishuhudia shule kufungwa, hospitali kuharibiwa na uchumi kusimama.
Vijana waliopaswa kuwa madaktari, walimu au wahandisi walijikuta wakiwa wakimbizi au kujiunga na makundi yenye silaha. Huu ni ushahidi hai kwamba bila amani, rasilimali watu ambao ndio mtaji mkubwa wa maendeleo, hupotea.
Maendeleo ya Afrika yana uhusiano wa moja kwa moja na amani kwani baada ya nchi hupita katika vipindi vya migogoro na baadaye kufanikiwa kurejesha utulivu, uchumi ulianza kukua upya.
Katika mazingira ya amani, serikali huweza kupanga na kutekeleza sera za muda mrefu za maendeleo badala ya kutumia rasilimali nyingi katika masuala ya ulinzi na usalama.
Hatua hiyo inaongeza kasi ya kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watu wa kawaida kama wakulima, wafanyabiashara wadogo na mfanyakazi wa kawaida.
AMANI NA UWEKEZAJI
Mwekezaji huangalia kwanza usalama wa mali na watu wake.
Ndiyo maana nchi zenye utulivu zimeendelea kuwa kivutio cha mitaji ya ndani na nje.
Viwanda hufunguliwa, ajira huongezeka na mapato ya serikali huimarika.
Kwa mantiki hiyo, amani siyo tu suala la usalama bali ni sera muhimu ya kiuchumi.
AMANI NA UMOJA WA JAMII
Afrika ni bara lenye mchanganyiko mkubwa wa makabila, lugha na tamaduni.
Amani huwezesha tofauti hizo kuwa chanzo cha utajiri wa kijamii badala ya migawanyiko.
Pale ambapo mazungumzo na maridhiano vinapewa kipaumbele, migogoro midogo ya kijamii hutatuliwa kabla haijageuka kuwa vita.
Hii inaonesha kuwa amani hujengwa kila siku kupitia uvumilivu, haki na usawa.
NAFASI YA TAASISI ZA KIKANDA
Juhudi za kulinda amani barani Afrika zimekuwa zikihusisha taasisi za kikanda kama Umoja wa Afrika (AU) pamoja na mashirika ya kimataifa.
Kupitia usuluhishi, uangalizi wa uchaguzi na operesheni za kulinda amani, taasisi hizo zimechangia kuzuia migogoro na kurejesha utulivu katika maeneo tete.
Hata hivyo, suluhu ya kudumu lazima itokane na Waafrika wenyewe kwa kuheshimu haki, katiba na utawala bora.
AMANI NA VIJANA
Takwimu zinabainisha kuwa zaidi ya nusu ya idadi ya watu Afrika ni vijana.
Amani huwapa vijana fursa ya kusoma, kubuni na kushiriki kikamilifu katika uchumi. Bila amani, vijana hugeuka kuwa waathirika wakuu wa vita, wakikosa elimu, ajira na matumaini.
Kuwekeza katika amani ni sawa na kuwekeza katika nguvu kazi kwani amani siyo kauli mbiu ya kisiasa bali ni ajenda ya maendeleo.
Afrika haiwezi kufikia malengo yake ya kiuchumi na kijamii bila kulinda na kudumisha amani. Kila raia, kuanzia kiongozi wa juu hadi mwananchi wa kawaida, ana wajibu wa kuilinda.
Afrika yenye amani ni Afrika yenye uwezo wa kusimama kifua mbele katika ushindani wa dunia na kuwapatia wananchi wake maisha yenye heshima na ustawi.





