Dodoma
Na Waandishi Wetu
HATUA ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza matumizi ya mafuta katika ofisi yake, imeelezwa ni ya kizalendo na kielelezo cha uongozi makini.
Katika hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Rais Dk. Samia aliwaagiza viongozi na watendaji serikalini, kupunguza matumizi ya mafuta, kufuatia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia, kunakotokana na vita vya Mashariki ya Kati.
“Ndani ya serikali tuna matumizi makubwa sana ya mafuta, magari ni mengi na safari ni nyingi, hivyo ni muhimu kuanza kupunguza matumizi,” alisema Rais Dk. Samia, katika tukio hilo ambalo Profesa Palamagamba Kabudi aliapishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, akichukua nafasi ya marehemu William Lukuvi.
Rais Dk. Samia alionyesha mfano alipotangaza kwamba kuanzia sasa, atakapokuwa anasafiri watendaji katika ofisi ya rais watakaofuatana naye, watatumia usafiri wa pamoja wa mabasi madogo, hatua itakayopunguza matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji.
Wabunge, wasomi na wananchi kwa jumla, wamepongeza uamuzi huo wa Dk. Samia wakieleza ni wa kizalendo na busara katika kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kuwa salama.
WABUNGE
Mbunge wa Kisarawe, Dk. Selemani Jafo, amesema Rais Dk. Samia ametoa somo la nini maana ya kuwa kiongozi makini na ana imani taifa litavuka salama dhidi ya changamoto ya bei ya mafuta kupaa.
“Nina imani tutatoka salama katika eneo hili na nchi itazidi kusonga mbele, tumuombee Mwenyezi Mungu amlinde katika utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Jafo.
Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa, amesema Rais, amefanya jambo la kizalendo na kutoa mwanga kama taifa nini kifanyike, akianza na ofisi yake kubana matumizi ya mafuta.
“Hii ndiyo maana ya uongozi wa kuonyesha njia.”alisema Mbunge Kadogosa.
Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe, ameeleza kuwa hatua ya Rais kuanza kubana matumizi ni uwajibikaji, kwa kuwa kuhusika na matatizo ya Watanzania ni kujali kwa kiongozi.
“Haijalishi ni kwa kiwango gani tutapunguza matumizi ya mafuta, lakini kwa kiongozi mkuu kufanya hivyo kwa vitendo, ni kuagiza taifa lote kuishi kwa kufunga mkanda kipindi hiki cha uhaba wa mafuta. Ni matarajio yangu serikali na taasisi zake watapunguza matumizi ya mafuta,”alisema.
Mbunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu, alisema kitendo cha Rais kupunguza idadi ya magari katika safari zake ni cha kizalendo na mapenzi kwa nchi.
“Rais ameonesha kuguswa na jambo la matumizi serikalini, wakati huu ambapo wananchi wanaenda kuwa na mzigo wa uzalishaji kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani, nimefarijika sana,” amesema mbunge huyo.
Alisema wananchi wanapenda kuona viongozi wanaguswa na hisia zao na maumivu yao, kwa hiyo uamuzi huo wa Rais Dk. Samia hapana budi ufuatwe na viongozi na watendaji wote serikalini.
Kingu alishauri utolewe waraka wa serikali utakaowaelekeza viongozi wakiwemo wa kitaifa, mawaziri na wakuu wa mikoa kubana matumizi kwa kuhakikisha misafara yao inaepukana na msururu wa magari.
“Siku zote tunasema Rais Samia ni msikivu na anajali shida za watu anaowaongoza, nimefarijika kwa sababu mimi naona Rais amejibu kwa matendo, huu ndiyo uongozi, angalia namna wananchi wamepokea kwenye mitandao, hii inajenga imani kubwa ya wananchi kwa uongozi wa nchi yao,” alisema Kingu.
Mbunge wa Mbeya Vijijini, Patali Shida Patali, amesema hatua ya Rais Samia ya kutangaza kubana matumizi ni mtazamo mpya wa utawala bora kwa nchi.
Mchumi Dk. Hildebrand Shayo, amesema uamuzi wa Rais Dk. Samia wa kuanza kupunguza matumizi ya mafuta kupitia magari ya msafara wake ni nzuri.
Alisema hatua kubana matumizi kukabiliana na changamoto ya kupaa kwa bei ya bidhaa za petroli, isiwe kwa viongozi na watendaji serikalini pekee, hata walio katika sekta binafsi wapunguze safari zisizo za lazima.
“Rais Dk. Samia ameamua kuanza na ‘nyumbani’ ni jambo zuri ambalo linatakiwa kuungwa mkono na watu wengine hata wa sekta binfsi ili kupunguza matumizi ya mafuta kwa wingi,” alishauri msomi huyo.
WANANCHI
Juma Mfaume, mkazi wa Mipango mjini Dodoma, alisema uamuzi wa rais unaonesha mfano wa uongozi wa vitendo na uzalendo kwa taifa.
“Hii ni ishara nzuri sana. Kama Rais mwenyewe anaweza kupunguza matumizi, basi hata viongozi wengine wanapaswa kuiga,” alisema.
Mfanyabiashara ndogo ndogo katika Soko la Majengo, Rehema Said;
“Tunapambana na hali ngumu ya maisha, tukiona viongozi wanapunguza matumizi tunajisikia kuthaminiwa. Ina maana wanawafikiria wananchi.”




