Na MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amefichua kuwa ana kipaji cha kucheza soka na wakati yupo shuleni alikuwa akisakata mpira wa miguu.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipozungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ikulu, Zanzibar.
Alisema majukumu ya taaluma ya udaktari na baadaye nafasi ya Urais yamechangia kumfanya asiendelee kushiriki mchezo huo kwa muda mrefu, licha ya kuendelea kuwa na mapenzi makubwa na mpira wa miguu.
Dk. Mwinyi alisema alipokuwa akisakata soka, alikuwa mchezaji mwenye kipaji kizuri.
“Mimi nilivyokuwa shule nilikuwa mchezaji wa mpira wa miguu na nilikuwa mchezaji mzuri sana, lakini baada ya kuingia katika maswala ya kazi haya toka niingie katika maswala ya udaktari nilikuwa nashughulika sana na kazi, kwa hiyo nikaacha muda mrefu na baada ya hapo nikaingia kwenye siasa muda haukupatikana kabisa, lakini mara moja moja tukiwa bungeni nilikuwa ninacheza,” alisema.
Kuhusu kuhusishwa na ushabiki wa klabu ya Simba au Yanga, Dk. Mwinyi alisema hajawahi kujitambulisha kuwa upande wowote.
Amesema mara nyingi amekuwa akiulizwa kuhusu timu anayoishabikia, lakini hajawahi kuweka wazi msimamo wake, akisisitiza kwa utani kuwa, “katika hilo wamenitafuta sana hawajanipata, na wewe leo hunipati.” Dk. Mwinyi alimwambia mwandishi wa TBC huku akitabasamu.




