Na REHEMA MAIGALA
MSANII wa Bongo Fleva na Mjasiriamali, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, baada ya kusema kuwa hatawaangusha wafanyabiashara wa vyakula ‘Mamalishe’.
Pia, alisema ushiriki wake katika kongamano la Kitaifa la Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), lililofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, jana, limepandisha hadhi zao na shughuli zao kwa ujumla.
Akizungumza na UHURU , Shilole alisema Rais Samia ni kiongozi mbunifu mwenye nia ya kuwapa faraja wafanyabiashara wadogo na kutaka wakue kiuchumi.
“Rais Samia anajua changamoto za mama na babalishe na ndio maana ameahidi kuwa nao beba kwa bega, kuhakikisha wanafanya shughuli zao katika mazingira yaliyo bora,” alisema Shilole.
Aliongeza kuwa, kauli hiyo aliitoa Rais kuwa hatowaangusha imeleta faraja kubwa na kuwapa nguvu zaidi ya kufanya kazi pamoja na changamoto nyingi.
Msanii huyo alisema amefurahi kushiriki kongamano ushiriki wake katika kongamano hilo ni kutaka kuona kila kitu kinaenda sawa kwa baba na mamalishe.
“Tunachangamoto nyingi katika kazi zetu hasa za kufukuzwa mara kwa mara na askari wa jiji katika sehemu tunazofanyia biashara, hukusanya vyakula na vyombo na kuondoka navyo na kutuacha tukiwa hatuna mitaji wala vyombo vya kupikia,” aliongeza.
Hata hivyo, Shilole alisema kwa kuwa tayari baadhi ya kero wamezitoa kwa Rais, anaamini mambo yatakuwa sawa.
Juzi Rais Dk. Samia alisema hatawaangusha mama na babalishe kutokana na mchango wao mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema kundi hilo ni muhimu katika jamii, hivyo ataboresha kazi zao na kutatua changamoto zinazowakabili ili wafanye kazi kwa ufanisi na kukuza uchumi wa nchi.




