Na HANIFA RAMADHANI, Zanzibar
TIMU za soka za Simba na Mafunzo zinatarajiwa kupambana leo katika michuano ya Kombe la Muungano utakaopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Mchezo huo, tayari umevuta hisia za mashabiki wengi wa soka, umepangwa kuanza majira ya saa 1:15 usiku.
Wakizungumza jana, Amani mjini Unguja, makocha wa timu hizo wamesema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo.
Kocha wa timu ya Simba, Steve Barker alisema, wamekuja Zanzibar katika michuano hiyo kwa malengo makuu matatu, ikiwemo kushinda ubingwa wa mashindano hayo.
Alisema lengo la pili ni kutoa fursa kwa wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mengine.
Pia, alisema lengo la tatu ni kujijenga upya kiakili kabla ya kuendelea na ratiba ngumu ya ligi kuu.
Kwa upande wake, Kocha wa timu ya Mafunzo, Haji Ramadhan Mwambe alisema Simba ni timu kubwa lakini na wao wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo.
“Tunajua kwamba tunakutana na timu kubwa yenye wachezaji wakubwa,lakini sisi mafunzo tumejiandaa vizuri kushinda,” alisema.
Alieleza kuwa, timu yake ina wachezaji wazuri na vijana ambao wapo tayari kucheza na Simba.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Shomari Kapombe alisema wamejiandaa vizuri na mchezo huo na kwamba wamekuja Zanzibar kushindana.
Alisema, malengo siyo kushiriki tu bali ni kushinda taji hilo la Kombe la Muungano kwa mwaka huu.




