Na REHEMA MAIGALA
WASOMI na mwanasiasa, wameelezea manufaa ya mkakati wa serikali kutoza sh. 10 kila kilo moja ya sukari kwa lengo la kuwasilishwa katika Mfuko wa Bima ya Afya, wananchi wengi wapate huduma hiyo kwa urahisi.
Wamesema mbinu hiyo, itasaidia Watanzania wengi kupata huduma nzuri na kwa gharama nafuu.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, Alhamisi Juni 11, 2026, alitangaza hatua mpya za kimkakati kupunguza matumizi ya fedha taslimu, kuanzia Mwaka wa Fedha 2026/2027, zikiwa ni jitihada za kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza uwazi katika miamala ya fedha.
Balozi Omar alitangaza hatua hiyo alipowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, jana, wanasiasa na wasomi hao, waliipongeza serikali kwa mkakati huo ambao utakuwa msaada mkubwa kwa Watanzania katika suala zima la afya.
DK. PHILIP DANINGA
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi na Uongozi wa Chuo Cha Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga, aliunga mkono hatua ya serikali ya kutaka kukusanya sh. Bilioni 7.5 kupitia vyanzo vipya vya mapato vitakavyowezesha kugharamia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Dk. Daninga, alisema huduma ya bima ya afya ni kitu muhimu kwa afya ya binadamu, ambayo itamwezesha mtumiaji kutumia fedha kidogo na kupata huduma kwa gharama nzuri na salama kwa afya yake.
Alisema serikali imeamua kubuni mkakati huo kwa upande wa bima ya afya, lengo ni kutaka kuwasaidia wananchi katika upande wa sekta ya afya baada ya gharama za huduma za matibabu kuwa juu.
“Mpango huu utakuwa mkombozi kwa Watanzania wengi, kwa sababu hadi leo hii, wapo baadhi ya watu wanapata maradhi, wanashindwa kwenda hospitali kwa kutokidhi gharama za matibabu.
Hivyo, kama kila mwananchi atakuwa na kadi yake ya bima ya afya, itarahisisha watu kupata huduma nzuri na bei nafuu,” alisema.
Dk. Daninga, alisema mtaji mkubwa wa binadamu ni afya njema, ambayo itamsaidia kufanya shughuli zake za uzalishaji mali.
DK. SYLVESTER RUGEIHYAM
Mtaalamu wa Somo la Hisabati na Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sylvester Rugeihyam, aliipongeza serikali kwa mkakati mzuri wa kuwapatia wananchi huduma ya afya.
Dk. Rugeihyam, alisema kupitia tozo ya sh. 10 kwa kila kilo moja ya sukari, serikali imerahisisha na lengo lake ni kutaka kila mwananchi apate huduma ya bima ya afya. tofauti na ilivyo hivi sasa.
“Ubunifu huu, utawasaidia wananchi wengi wakiwemo wa kipato cha chini na kati, wote hao watapata huduma bora ya bima ya afya,”alisema.
HASSAN DOYO
Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Hassan Doyo, alisema ubunifu mpya katika vyanzo vya mapato ni miongoni mwa maendeleo nchini.
“Naipongeza serikali kwa ubunifu huo ambao utawarahisishia wananchi wengi kupata huduma ya afya,”alisema.
Doyo alipendekeza kuwa, huduma hiyo ya bima ya afya iendelee kudumu ni vyema serikali ingetoza sh. 100 kwa kila kilo 100 ya mahindi.
“Ubunifu huu wananchi wameufurahia tangu wausikie tunachoomba tunataka ufanikiwe na kila Mtanzania afaidie na mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote,”alisema.
PILI MSELU
Mkazi Kinondoni Dar es Salaam, Pili Mselu, alisema mikakati inayofanywa na serikali ya kutaka kila Mtanzania awe na bima ya afya imekuwa ni mkombozi kwake na watanzania wengine.
Mwishoni mwa wiki, Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Omar, alisema serikali inatarajia kukusanya sh. bilioni 7.5 kupitia vyanzo vipya vya mapato.
Balozi Omar alisema hayo bungeni, alipotangaza mkakati huo alipowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Alisema hatua hiyo inatokana na mapendekezo ya sheria na kanuni yanayolenga kuongeza uwezo wa kifedha wa serikali katika sekta ya afya.




