SALVATORY NTANDU, Shinyanga
MKAZI wa Kijiji cha Lyabukande, Bundala Mashiku, amekamatwa kwa tuhuma za kuoa mwanafunzi wa kidato cha tano kwa ahadi ya mahari ya sh. milioni 4.5.
Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Julias Mtatiro, ilimkamata Bundala (24), ambaye alitarajia kulipa mahari hiyo Agosti 5, mwaka huu.
Akizungumza katika msako huo, Mtatiro alisema mwanafunzi huyo alichaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Kili iliyopo wilayani Nzega Mkoa wa Tabora, ambapo wazazi wake walimwozesha kwa familia ya Mashiku Sylivesta.
Alisema serikali haitavumilia kuona uozeshaji wanafunzi ukiendelea, hivyo Bundala, baba yake Mashiku, watashikiliwa na vyombo vya usalama na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
“Natangaza vita kwa wazazi ambao wameozesha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, tunaendelea na msako wa kila familia ili kuhakikisha wote waliochaguliwa wanaenda shule kutimiza ndoto zao,”alisema Mtatiro.
Aidha, Mtatiro aliwataka wazazi kuacha tamaa ya mali kuozesha wanafunzi kwa kuwa sheria zipo na zinaendelea kufanya kazi.
“Watakaobainika watakamatwa na kufikishwa mahakamani kitendo hiki hakifai kuigwa katika jamii na kila mwananchi anapaswa kukikemea,” alisema Mtatiro.
Kwa upande wake, Mashiku alidai hakujua kama binti huyo ni mwanafunzi na alikubaliana kulipa mahari ya sh. milioni tatu Agosti 5 na mwakani angemalizia sh. milioni 1.5, baada ya kuishi nyumbani kwake miezi miwili.
“Kijana wangu alichumbia mke akamleta nyumbani, familia tukakubaliana kulipa mahari. Sikujua kama ni mwanafunzi nilifahamu alimaliza kidato cha nne mwaka jana sikuwa na wasiwasi,”alisema.
Awali, Bundala alidai hakuwa akifahamu kama mke wake ni mwanafunzi aliyefaulu kujiunga na kidato cha tano.




