Na AMINA KASHEBA
SAA chache baada ya timu ya Azam FC kuondoka nchini kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), nyota wa timu hiyo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameahidi watapambana kupata ushindi.
Azam itakuwa ugenini Jumapili kumenyana na As Maniema katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya CAFCC utakaochezwa nchini Congo.
Akizungumza kabla ya kuondoka nchini jana, Fei Toto alisema wataingia katika mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani wao kwani wanaamini mechi itakuwa na upinzani mkubwa.
“Tunakwenda katika mchezo mgumu lakini tutawaheshimu wapinzani wetu na siyo kuwaogopa, tumejipanga vyema na hatuna presha yeyote tunakwenda kupambana kupata matokeo mazuri,” alisema.
Fei aliwaomba mashabiki waendelee kuwasapoti na kuiombea timu yao kuhakikisha wanapata ushindi na kuiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele.
“Mashabiki waendelee kutuombea dua kwani sisi tunakwenda kuwapa furaha maombi yao ni muhimu kwetu katika mchezo uliopo mbele yetu,” alisema.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Hashim Ibwe alisema wachezaji wao wamejiandaa vizuri kuwakabili wapinzani wao.
“Kocha Florent Ibenge na benchi lake la ufundi wamefanya kazi kubwa katika viwanja vya mazoezi, hivyo tuna imani wachezaji watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri,” alisema Ibwe.
Azam wapo kundi B wakiwa na timu za Wydad AC ya Morocco, AS Maniema Union ya (DRC) na Nairobi United ya Kenya.




