Dodoma
NA MWANDISHI WETU
JUKWAA la Wanawake Tanzania limeazimia mambo 10 yenye lengo la kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kuilinda amani iliyopo huku likimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha utulivu nchini.
Maazimio hayo yametolewa jijini hapa na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Zainab Shomari katika kongamano la Jukwaa la Wanawake 2025.
Amesema azimio la kwanza ni jukwaa hilo kuendelea kuwa sehemu ya ujenzi wa amani ya kudumu kwa kuimarisha majadiliano na maridhiano yenye kujenga jamii kwani mazungumzo ya wazi ndiyo uimarisha mshikamano.
Pia, amesema azimio la tatu ni kuendeleza matumizi salama yenye uadilifu ya mitandao ya kidijitali kwa kutumia maudhui yenye kukuza umoja, kuheshimiana, ustaarabu na kutunza taswira ya Taifa.
Azimio la nne lililofikiwa katika jukwaa hilo lililowakutanisha washiriki zaidi ya 2000 ni kuhamasisha, kuongeza fursa za maendeleo kwa wanawake na vijana katika maeneo mbalimbali ya jamii.
“Azimio la tano ni kujizatiti katika kuelimisha jamii yetu kuhusu maadili, utu, uzalendo na utatuzi wa migogoro kwa njia za hekima kwa kuwa hivi ndivyo vinavyoijenga Tanzania kuwa taifa linalosikilizana, kuvumiliana na linaloheshimu umoja wetu.
“Tukiwa nguzo ya malezi, tuna wajibu wa kuandaa vizazi vinavyothamini amani kama sehemu ya utambulisho wa taifa letu,” alisema Shomari.
Amesema azimio la sita ni kukubali wajibu wao katika kutimiza ndoto ya Tanzania waitakayo kwani Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, imeweka bayana kwamba amani ni msingi wa uchumi jumuishi na shindani.
Vilevile, amesema azimio la sita ni kujitolea kwa dhati kushiriki kikamilifu kuilinda na kuiendeleza amani kwa vitendo.
Pia, katika azimio la saba kongamano hilo lilimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hatua zote alizochukua kurejesha hali ya amani na utulivu nchini.
Zainab amesema azimio la nane ni kuunga mkono uteuzi wa Tume ya Uchunguzi ili kuweka mazingira mazuri ya kuwepo maridhiano na maelewano nchini.
Azimio la tisa ambalo kongamano hilo lilikuja nalo ni kwamba wanawake nchini wataendelea kuwa sehemu muhimu ya ustawi wa taifa kwa kuzingatia hekima, utulivu na umoja.
“Tunatoa neno la faraja kuonesha mshikamano na wote ambao walipitia kadhia hiyo. Tukiwa sauti ya amani, tunathamini utulivu na tunaunga mkono hatua ya Rais Dk. Samia kuunda Tume ya Uchunguzi kwa lengo la kupata ukweli, kuweka misingi ya maelewano na kuimarisha umoja wa taifa,” amebainisha.
Katika azimio la kumi, kongamano hilo lilitoa wito kwa Watanzania hususan vijana kuhakikisha wanaendelea kudumisha amani na kujenga mazingira ya kutumia mazungumzo, majadiliano na maridhiano.




