Na JOE NAKAJUMO
KATIKA bara la Afrika,Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeweka rekodi ya kuwa Chama kikongwe. Wiki ijayo, Februari 5, kitatimiza umri wa karibu nusu karne.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitakuwa kinasherehekea miaka 49 tangu kuundwa kwake Februari 5, mwaka 1977. Miaka hii siyo michache, kwani inafikia umri wa mtu mzima.
Kwa miaka yote hii, tangu kuundwa kwake, CCM, imemudu kuunda serikali katika pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar.
UKOMAVU WA CCM
Swali linakuja, CCM, imewezaje kuwa imara miaka yote hii na muda wote kushika dola. Mshikamano na umoja miongoni mwa wanachama wake. CCM, imejiwekea msingi wa mizizi imara ya uongozi kuanzia ngazi ya chini na kuifanya iwe na ukomavu. Hili ni jibu la swali.
Ushahidi wa uwepo mshikamano na umoja, unaonekana wakati wa uchaguzi,uwe wa Chama au Serikali. Wagombea wa CCM wanapigana vikumbo wakati wa kampeni,matokeo yakishatangazwa na kumpata mshindi,wanarudi kwenye umoja wao. Aliyeshindwa anampongeza aliyeshinda bila kinyongo.
Baada ya uchaguzi,inatolewa ilani ya kuvunjwa makundi na wanachama kwa nidhamu wanarudi kuwa na mshikamano na umoja. Hivyo,kizazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, kimelelewa, kuishi kwa misingi ya mshikamano, umoja na amani.
ZIARA DAR ES SALAAM
Mapema mwezi huu wa Januari, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, alifanya ziara ya Chama, mkoani Dar es Salaam. Unaweza kuitaja kuwa ilikuwa ziara ya kuimarisha uhai wa Chama. Alifanya mikutano na viongozi wa mashina ya Chama na mabalozi.
Katika mikutano na viongozi hawa wa ngazi ya chini, Katibu Mkuu, alieleza na kuhimiza umuhimu wa vikao vya mashina, mabalozi na wanachama katika maeneo yao ikiwa moja ya hatua za kuimarisha Chama.
Dk. Migiro, aliwataka makatibu wa itikadi na uenezi,kushirikiana na viongozi wa mashina katika madarasa ya itikadi. Aliongeza kwamba mashina ndiyo darasa la kwanza la itikadi na wanachama watajifunza misingi ya CCM.
Sina hakika kama unaendelea utaratibu wa zamani wa mtu anayeomba kujiunga na CCM, anapaswa kwanza kuhudhuria masomo ya itikadi kwenye shina au tawi. Ni vizuri Katibu Mkuu, amekumbusha umuhimu wa madarasa ya itikadi.
UHAI WA CHAMA
Dk. Migoro anasema uhai wa Chama Cha Mapinduzi, unatokana na mashina na kwamba kupitia vikao, Chama kinaweza kujipima kina uwezo kiasi gani. Hivyo anasisitiza kufanyika kwa vikao na ni wajibu wa kila mwanachama, hasa viongozi kushiriki kikamilifu kwenye vikao.
Anafafanua kwamba ndani ya vikao kuna kubadilishana uzoefu na zitakuwepo taarifa sahihi za kukisukuma Chama Cha Mapinduzi ngazi zinazofuata.”
Mashina ndiyo darasa la kwanza la itikadi, kupitia mashina haya, kizazi kitajifunza historia ya Chama Cha Mapinduzi, historia ya nchi yetu na maana ya kuwa mwanaCCM,”anasisitiza Katibu Mkuu wa Chama.
MAAGIZO WABUNGE NA MAWAZIRI
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CCM, ametoa maagizo kwa wabunge na mawaziri, kuhudhuria vikao vya ngazi ya mashina, kubaini changamoto zinazowakabili wananchi. Hatua hii, anasema ,itawawezesha wabunge na mawaziri kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali, zitakazoibuliwa katika vikao.
Anakumbusha kuwepo wabunge na mawaziri kwenye vikao vya mashina, kutawawezesha kubaini changamoto walizoahidi kuzifanyia kazi katika Ilani ya Uchaguzi, baada ya kupokea dola. Anasema mabalozi wa mashina ni chemichemi ya fikra, macho, masikio na daraja linalounganisha Chama na wananchi.
“Viongozi wa ngazi za juu,tufanye vikao vya kikatiba kupata changamoto za wananchi na tushauri Chama ili kuishauri Serikali,”anasisitiza Katibu Mkuu wa CCM.
TANU MWAKA 1966
Umuhimu wa mawaziri kuhudhuria vikao vya chini vya Chama,ulianza kusisitizwa tangu enzi za TANU. Oktoba, mwaka 1966, Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU, iliwataka mawaziri kufungua ofisi katika ofisi za Chama,ili shida za wananchi zisikike.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU katika mkutano wake wa siku moja,uliofanyika Dar es Salaam,Oktoba Mosi,mwaka 1966,iliagiza kwamba mawaziri wote wa serikali sasa itawabidi kuwa na ofisi zao katika Ofisi Kuu ya TANU ambako watakuwa wakionana na wananchi kusikiliza shida zao.
AGIZO KWA MAWAZIRI
Halmashauri Kuu, iliwataka mawaziri wote,wakishirikiana na Ofisi Kuu ya TANU, wapange utaratibu na siku maalum, watakazokuwepo katika ofisi hizo mpya kungojea kusikiliza shida za wananchi.
Taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya TANU, ilisema kuwa azimio hili pia linawahusu wakuu wa mikoa na wilaya ambao watafanya utaratibu maalumu wa kuwa na ofisi zao katika ofisi za TANU, watakaokuwa wanasikiliza shida za wananchi. Hawa watakuwa wanashirikiana na Mwenyekiti wa Chama katika kuonana na kusikiliza shida za wananchi.
Taarifa ya Makao Makuu ya Chama, imekumbusha kuwa Serikali ni chombo cha wananchi cha kufanya na kutimiza kazi na kwamba TANU ndiyo watu wenyewe na kwa hivyo ofisi za TANU ndiyo mahali pa wananchi kuwasilisha shida na mashauri yao.
MAELEKEZO YA DK.SAMIA
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, mara kwa mara katika majukwaa mbalimbali amekuwa akiwahimiza viongozi kushuka chini kukutana na wananchi kujua kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Mwezi Agosti, mwaka jana 2025, katika hafla ya kuwaapisha viongozi,Ikulu Chamwino, Dodoma, Rais Dk.Samia, alitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa nchini kusikiliza na kutatua kero za wananchi wanaowaongoza.
Dk. Samia alitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi kuzifahamu kero wanazokabiliwa nazo na kuzitafutia suluhu kwa kushirikiana na watendaji wengine.
KATIBU WA NEC
Novemba mwaka jana, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alisema Chama Cha Mapinduzi, kitaisimamia serikali na hakitasita kuwachukulia hatua viongozi wavivu, wazembe na watakaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema kile ambacho Watanzania waliahidiwa, lazima kitekelezwe, hivyo viongozi wanapaswa kuwajibika ipasavyo na wataweka vipimo vya uwajibikaji na utendaji kazi wa viongozi wa serikali kwa kuchekecha utendaji wao.
“Yule ambaye ufanisi wake utakuwa ni chini, Chama kitachukua hatua mara moja. Wale watakaofanya vizuri, Chama kitaendelea kuwalinda kuhakikisha kazi yenye matunda mema kwa Watanzania inafanikiwa,” alisisitiza Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo.
Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, 2025—2030, kupitia ahadi za mgombea, Kihongosi aliwataka mawaziri na naibu mawaziri kutambua kuwa wajibu wa Chama ni kuisimamia serikali, siyo serikali kukisimamia Chama. Kazi imeanza,Chama kitaifuatilia serikali kuhakikisha yaliyoahidiwa katika kampeni yanatekelezwa.
BABA WA TAIFA
Oktoba mwaka 1976, Baba wa Taifa, Rais Mwalimu Julius Nyerere, alisema serikali ni madaraka ya utawala na hutumia madaraka hayo kwa kupitia vyombo vilivyowekwa, wakati Chama ni umoja wa wananchi waliojiunga kwa madhumuni maalumu na mara nyingi kwa shabaha ya kushika serikali ili itumiwe kutekeleza maslahi ya wananchi.
Mwalimu Nyerere alisema mara nyingi, serikali huogopwa kinyume na Chama ambacho lugha yake ni kueleza, kuelekeza na kuongoza kwa sababu Chama kinatokana na watu na ni cha watu wenyewe. (Mawasiliano na Mwandishi WhatsApp 0784291434;email nakajumoj@gmail.com)




