Na Fred Alfred
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ameipa Wizara ya Maji siku 14 kuhakikisha inakamilisha mchakato wa upatikanaji wa Mkandarasi wa ujenzi wa maji kutoka chanzo cha ziwa Chala.
Dk. Mwigulu aliyasema hayo katika muendelezo wa ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Amesema ujenzi wa mradi huo unapaswa kuanza kutekelezwa kwani unategemewa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya nzima ya Rombo.
“Natoa wiki mbili kwa wizara ya maji kuhakikisha inakamilisha mchakato wa upatikanaji wa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha Ziwa Chala.Mradi wa maji ziwa Chala unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh.bilioni 8.6 na utanufaisha wananchi 34,104 katika vijiji 14 vya wilaya ya Rombo,”amesema.
ATAKA KUSIKILIZA WANANCHI
Katika hatua nyingine, Dk.Mwigulu aliwataka watumishi wa umma wanaopuuza kero za wananchi huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi yao.
Amesema ni muhimu watmishi kuacha kukaa ofisini bali wawafikiue wananchi na kutatua kero zao.
“Bado tunaendelea kupambana na wananchi wanaopuuza sauti za wananchi. Lengo la serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia ni kuona wanafanya kazi kwa uzalendo na uaminifu.
Ameongeza kuwa :”Tutaendelea kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wazembe na wabadhilifu.
BARABARA
Kadhalika, Dk. Mwigulu amemuagiza Waziri wa Fedha kuhakikisha anatafuta fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya awali kwa mkandarasi ili aanze ujenzi wa mradi wa barabara Holili (Rotima)-Tarakea(Nayemi) kilomita 52.8
Alisema Mradi huo ambao utagharimu kiasi cha sh. bilioni 28 unapita mpakani mwa Tanzania na Kenya na unategemewa kusaidia kukuza shughuli za kijamii, kiuchumi pamoja na utalii.
“Barabara hii ni muhimu kiuchumi na kibiashara kwasababu inaunganisha nchi mbili hivyo lazima tuhakikishe fedha zinapatikana kwa wakati kwa ajili ya kuanza ujenzi wake,”alisema
SHULE
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Stephen Moshi Technical ambayo itagharimu sh. bilioni 1.6 Dk. Mwigulu alisema kuwa shule hiyo ni kielelezo cha uwepo wa kiongozi mwenye maono na mipango.
“Ndani ya muda mchache sana zimejengwa shule zaidi ya 103 za aina hii nchi nzima” Alisema Dk. Mwigulu.
Aliongeza kuwa :“Rais Dk.Samia tangu ameingia madarakani amejenga shule 1300 na madarasa 79000 ili kiuhakikisha watoto wanapata elimu bila vikwazo.
Vilevile ndani ya siku 100 ameajiri walimu 7000 na kupelekwa katika vituo vya kazi kwa ajili ya kufundisha.
MIRADI YA KIMKAKATI
Dk. Mwigulu alisema Rais Dk.Samia ameendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati nchini.
Alisema miradi hiyo ni chachu ya maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Hivi sasa ni Tanzania pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki ambayo ina umeme wa ziada zaidi ya megawati 2000 baada ya kukamilisha ujenzi wa bwawa la mwalimu nyerere.
Aliongeza kuwa :”Kazi yangu kama msimamizi wa serikali ni kuhakikisha maono ya Rais Dk. Samia yanatekelezwa kwa weledi na kikamilifu. Kila aliyepewa jukumu la kusimamia shughuli za serilaki atekeleze kwa umakini na weredi mkubwa.
AWESO
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kuwa Wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo na watahakikisha katika kipindi cha siku 14 wanampata mkandarasi wa mradi huo.
Alisema Rais Dk.Samia alipoingia madarakani aliahidi kumtua mama ndoo kichwani na kampeni hiyo ameitekeleza kikamilifu.
“Ndugu zangu niwahakikishie kuwa tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi mnapata maji ya kutosha ili kuendelea kutimiza adhma ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama bila vikwazo.
WAZIRI MKENDA
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imeenda sambamba na ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk.Samia.
Alisema ziara hiyo iumeleta moshi mweupe katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.
“Rombo tulikuwa na vituo vinne vya afya lakini hadi sasa vimefika nane hiyo ni hatua kubwa ambayo tunahitaji kumpongeza Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika wilaya zetu,”alisema Mkenda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo.




