Na MWANDISHI MAALUMU
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema serikali inatambua uwepo wa watumishi wa umma wanaofanya kazi vizuri.
Dk. Mwigulu aliwataka watumishi waadilifu kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujiepusha kujiingiza katika makundi ya wazembe, wezi na wanaofanya kazi kwa mazoea.
“Serikali haitomuonea mtu, watumishi wachapakazi wasiingie ubaridi kwa sababu serikali inatambua mchango wao katika maendeleo ya taifa. Watu wasome alama za nyakati serikali haitovumilia masuala ya wizi kwa sababu yanarudisha nyuma maendeleo,” alisema.
Dk. Mwigulu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Aliwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi na kuepuka udokozi kwa sababu haukubaliki na hauvimiliki.
Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma watekeleze majukumu yao kwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa miradi.
UCHIMBAJI VISIMA
Pia, alisisitiza mikoa yote kuhakikisha katika upangaji wa bajeti, wanaweka vipaumbele vya uchimbaji visima kupitia mitambo iliyosambazwa katika mikoa yao.
“Mitambo ya uchimbaji maji itumike kuchimba visima wananchi wapate maji ya uhakika,” alisema Dk. Mwigulu.
Aidha, alizitaka mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu au sheria itakayowabana wakandarasi kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi wao stahiki kwa wakati.
Waziri Mkuu Mwigulu alitoa agizo hilo kufuatia kuwepo malalamiko kwa baadhi ya wakandarasi, kutowalipa wafanyakazi wao katika miradi ya ujenzi.
Alitoa agizo hilo baada ya wananchi waliofanya kazi katika miradi mbalimbali, kueleza kero ya kutolipwa japokuwa wakandarasi hao tayari serikali imewalipa.
WABUNGE MKOANI RUKWA
Baadhi ya wabunge wa mkoa wa Rukwa waliipongeza serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ikiwemo ya afya, elimu na kilimo.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini Salum Kazukamwe alisema ujenzi wa Hospitali ya Wilaya utarahisisha upatikanaji huduma bora za afya.




