VICTOR MKUMBO, Morocco Na AMINA KASHEBA
TIMU ya Taifa ya Serengeti Boys, im emwagiwa salamu za pongezi kwa kujituma, kuweka mbele uzalendo hadi kufika fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON U-17).
Serengeti boys inayoundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 17, jana usiku ilipepetana na Senegal katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Moulay Hassan, Rabat nchini Morocco.
Timu hiyo inayonolewa na kocha elieneza Nsanganzelu, ilifuzu fainali baada ya kuifunga Misri kwa penalti 4-3, katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa wiki iliyopita.
Pamoja na kucheza fainali, Serengeti Boys imeacha alama kubwa katika michuano hiyo baada ya wachezaji wake kutwaa tuzo tatu za mchezaji bora wa mechi huku ikiweka kibindoni mabao 10, yaliyopatikana katika mechi za hatua ya makundi, robo fainali na nusu fainali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, kutoka nchini Morocco na jijini Da res Salaam, wadau wa soka walisema wamefurahishwa na kile kilichooneshwa na wachezaji hao katika mashindano.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda alisema kuwa Rais Samia amewekeza katika michezo na matokeo yake yanaonekana.
“Rais Samia amefanya makubwa katika kuwekeza katika michezo, hivyo tunatakiwa kuilinda miundombinu ya michezo kwa ajili ya kuleta manufaa zaidi kwa wachezaji na Watanzania kwa ujumla.
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambaye anahudumia Morocco, Said Yakubu alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kuleta mashabiki wa kuipa saoti timu hiyo.
“Tunaipongeza Serengeti Boys, pia tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa kutuletea mashabiki kuongeza sapoti,” alisema.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema Serengeti Boys imefanya vizuri na kuiheshimisha Tanzania katika michuano hiyo kufuatia uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya michezo.
Mchezaji wa zamani, Zamoyoni Mogella, alisema Tanzania imeandika historia kubwa kupitia timu hiyo hivyo huu ni wakati wa kuwaendeleza wachezaji kwa lengo la kuwa na akiba ya timu ya taifa.
“Kuna benki za fedha, benki za damu lakini hii ni benki ya timu za taifa, hakuna sababu ya kuhangaika kutafuta timu ya taifa ijayo wakati tuna vijana wenye uwezo ambao wanaweza kupeperusha tena bendera ya nchin yetu,” alisema.
Kocha wa vijana, Maalim Salehe, aliishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa unaondelea kufanyika na kusisitiza kuwa mafanikio ya timu hiyo hayapaswi kuishia katika pongezi, bali yanapaswa kuwekewa programu maalumu.
Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),Lameck Nyambaya, alisema timu hiyo ikiendelezwa, kutunzwa yawezekana ikawa na faida kubwa katika siku za usoni kwani bado kuna mashindano mengi ambayo wanaweza kutumika.
Akizungumza baada ya kuwasili nchini Morocco, ambapo mashabiki wa soka waliokuja nchini Morocco, walipata nafasi ya kula chakula cha mchana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambaye anahudumia Morocco, Said Yakubu, katika Hoteli ya Sofitel, Rabat, Morocco, Nyambaya alisema baada ya timu hiyo kumaliza AFCON, wanapaswa kuandaliwa hiyo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar.
“Tayari Rais Dk. Samia alishaagiza kuwa vijana wanatakiwa kutunzwa, hivyo mamlaka husika tunatarajia zitazingatia hilo kuhakikisha malengo yanafikiwa, hawa vijana wamefanya kazi kubwa,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Taifa Stars Suppoters, Ziota Musisa ‘Papaa Ziota’ alisema anamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia kwani ameendelea kunyenyua michezo, tunaamini tutaendelea kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ambayo tutashiriki,” alisema Papaa Ziota.
Jerry Muro, ambaye yumo katika msafara wa wadau wa soka waliokuja Morocco kuisapoti timu, alisema sapoti anayotoa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika michezo, imeanza kuzaa matunda kwa asilimia 100.
Pia, wadau hao wamempongeza Rais Samia kwa kutoa ndege kwenda nchini Morocco, kutoa sapoti kwa wachezaji wa Serengeti Boys.
Mashabiki 200 na viongozi mbalimbali, waliwasili nchini humo kwa ajili ya kutoa sapoti katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Moulay Hassan, Rabat, Morocco.
Ofisa Habari wa TRA United, Christina Mwagala alisema kuwa mashabiki wamefurahishwa na kitendo cha kupewa ndege na Rais Samia.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kitendo cha kutupatia usafiri wa kuja hadi Morocco kwani ni suala la kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa,” alisema Christina.




