Na NASRA KITANA
WAKATI timu za Simba na Yanga zikitarajiwa kushuka dimbani wikiendi hii, timu hizo zinaingia uwanjani zikiwa kivingine huku kila upande ukitamba kuchukua alama tatu katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Michezo ya ligi hiyo, inatarajiwa kuendelea tena baada ya mapumziko ya wiki mbili huku kila timu ikipambana kuondoa kasoro zilizojitokeza katika mechi zilizopita.
Yanga inatarajiwa kuwa ugenini kesho kupambana na Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma huku Simba ikishuka dimbani keshokutwa katika mchezo wake dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Uwanja wa Meja Isamuhyo ikitaka kuendelea kuongoza michuano hiyo.
Akizungumza kuelekea katika mechi tano zilizobakia, kocha wa Yanga Abdihamid Moalin alisema timu yao inakuja kivingine kwa kupanga kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi zote zilizobakia wakianza na Mashujaa FC.
“Sisi kila mchezo ni kama fainali, wiki mbili za mapumziko tumepata nafasi ya kufanya marekebisho mapungufu yaliojitokeza ili kutimiza malengo tuliojiwekea. Pia tunajua tunaenda kupambana na Mashujaa ambayo ni timu bora na yenye wachezaji wazuri,” alisema Moalin.
Naye kocha wa Simba, Steve Barker alisema ana imani kubwa na timu yake kwa mechi tano zilizobakia kupata pointi tatu katika kila mchezo.
Barker alisema hawataki kuona wanapoteza mchezo wowote ule kwani malengo yao ni kuhakikisha wanabeba taji la ubingwa msimu huu wakianza na Pamba Jiji ambayo alisema siyo timu ya kuibeza.
“Malengo yetu ni kupata pointi tatu katika kila mchezo, hatutakubali kupoteza mchezo wowote ule uliokuwa mbele yetu hivyo tutahakikisha tunapambana kwa jasho na damu ili kupata ushindi,” alisema Barker.
Hata hivyo Barker alisema kuwa amefanya marekebisho katika kikosi chake ili kuweza kufanya vizuri.
Hadi sasa Yanga imebaki na mchezo dhidi ya Yanga ikibaki na mchezo dhidi ya Mashujaa FC, Fountain Gate FC, Azam FC, TRA United na JKT Tanzania huku Simba imebaki na mechi dhidi ya Pamba Jiji, Mbeya City, Mtibwa Sugar, Singida Black Stars na KMC.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 60 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 58 huku Azam ikishika nafasi ya tatu na pointi 52.




